WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa masomo 2023/2024 Serikali imetenga Sh. bilioni 48 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada.
Amesema hayo Jumanne, Januari 16, 2024 wakati wa ufunguzi wa Chuo Kikuu Katoliki Mbeya (CUoM) mkoani Mbeya.
Amesema kuwa mpango huo ambao ni maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unalenga kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kuwezesha wahitimu wa vyuo nchini kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na kimataifa.
“Lengo jingine la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kuona vijana wengi wanapata elimu itakayowapa ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Taifa”.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imetenga Dola za Kimarekani milioni moja kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambazo zinasomesha Wahadhiri 27 kutoka Vyuo Vikuu visivyo vya Serikali.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa fedha hizo pia zitatumika katika kugharamia wahadhiri saba katika ngazi ya Shahada ya Umahiri na 20 katika Shahada ya Uzamivu kwa programu za afya na sayansi shirikishi.
“Kupitia mradi huu Serikali imekuwa ikivifikia vyuo vikuu binafsi. Kitendo hicho kinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali yetu ya kuiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu kwa ngazi zote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi katika utaoaji wa elimu kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa vyuo vinavyomilikiwa na taasisi zisizo za Serikali kuweka mpango mkakati wa kuongeza idadi ya wanataaluma hususan maprofesa, wahadhiri waandamizi na wahadhiri kwa maeneo ya programu zinazotolewa.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inathamini na kutambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo Kanisa Katoliki kwa kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu na ustawi wa jamii.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi la Baraza la Chuo hicho Askofu John Ndimbo ameishukuru Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuona umuhimu wa kukipa chuo hicho hadhi ya chuo kikuu baada ya kutimiza masharti yote.
“Kupitia tume maalum iliyoundwa na Tume ya Vyuo Vikuu, ilijiridhisha na uboreshaji wa miundombinu ndipo tulipewa hadhi ya chuo kikuu, TCU imekuwa mlezi bora kwetu.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula ambaye amemuwakilisha Waziri wa Elimu kwenye ufunguzi huo, amelipongeza Kanisa Katoliki kwa namna linavyowekeza kwenye sekta ya elimu.
No comments:
Post a Comment