Tuesday, February 13, 2024

ALICHOZUNGUMZA KIKWETE MSIBANI KWA LOWASSA

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema anamfahamu Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kwa muda mrefu na wamekuwa pamoja tangu wakiwa Vijana na kisha kuwa Viongozi ambapo amesema mchango wa Lowassa kwa Taifa la Tanzania ni mkubwa.

Akiwa msibani kwa Lowassa Masaki Dar es salaam, Dkt. Kikwete amesema “Nimepokea kwa mshituko taarifa ya kifo, nilikuwa nafahamu kwamba anaumwa lakini sikutegemea kwamba ingefikia hapa ilipofikia, ninamfahamu marehemu kwa muda mrefu tulikuwa Vijana pamoja, tulikuwa Chuo Kikuu pamoja, tukatangulia sisi kuingia kwenye Chama na baadaye yeye akafuata na tumefanya kazi pamoja kwenye Chama kwa muda huo wote baadaye nikaendelea kwenye shughuli za Jeshi mwenzangu akaendelea kwenye shughuli za Chama, baadaye tukawa Wabunge na tukafika Baraza la Mawaziri”

“Mwaka 1995 siku moja asubuhi nikapokea ugeni Mtoto akaja chumbani akaniambia Baba kuna ugeni nikawakuta Marafiki zangu watatu, Kaka yangu Samuel Sitta, Edward Lowassa na Rostam Aziz, wakaja kuniambia kwamba Msemaji Samuel Sitta kwamba tunataka muende na Edward Dodoma mkachukue fomu ya kugombea Urais Mimi nikasema jambo hilo halipo kwenye mawazo yangu, kama yeye lipo kwenye mawazo basi aende, naye akasema siendi bila ya wewe”

“Basi tukabishana mpaka tukakubaliana kwamba wacha twende, tukaenda kuchukua fomu zile tukazijaza zikarudishwa, michakato ndani ya Chama mwenzangu hakubahatika Mimi nikabahatika kuwemo kati ya wale watano na baadaye tukapiga kura kwenye NEC nikawemo katika wale watatu, tukaenda mkutano mkuu nikawemo katika wawili lakini kura zangu hazikutosha akapata Mzee Mkapa nikaja kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje na mwenzangu akaja kuwa Waziri tena”

“2005 tukajiandaa na Mimi nikapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Rais mwenzangu akaja kuwa Waziri Mkuu tukapata changamoto katikati mwenzangu ikabidi akae pembeni, tumeendelea kuwa Marafiki tukishirikiana kwa kila linalowezekana, ameugua Mwenyezi Mungu amechukua roho yake, ninachoshauri tu tuendelee kumuombea, Mungu aipokee roho yake aiweke mahali pema peponi, Edward ametoa mchango mkubwa katika Taifa letu, yaliyotokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti yale mema na mazuri aliyolifanyia Taifa letu”


No comments: