Na WAF, DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk John Jingu amewataka wanataaluma wa Kada ya afya nchini kujenga tabia ya kutafuta maarifa mapya na kuboresha ujuzi ili kutoa huduma bora.
Dkt. Jingu ametoa rai hiyo Mei 10, 2024,Jijini Dodoma kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya mafunzo endelevu kwa wanataaluma wa Kada ya afya.
Dkt Jingu amesema wanataaluma wa Kada ya afya wanatakiwa kukuza utamaduni wa kujifunza ili kudumisha elimu na mtazamo unaotakiwa katika kutoa huduma bora.
"Kwenye mafunzo yenu tuhakikishe wataalamu wanakuwa na teknolojia zote itayowezesha kutoa huduma zenye ubora.
"Wekeni kipaumbele mafunzo endelevu kama sehemu muhimu ya maendeleo yenu ya kitaaluma hakikisheni mnabaki katika kasi na hali ya kujifunza kwa maendeleao ya taaluma," amesema Dkt Jingu.
Pia amewataka kutumia rasilimali zinazopatikana kama vile kozi za mtandaoni, mikutano ya kitaaluma, na vyanzo vingine vya kujifunza ili kuboresha maarifa, ujuzi na mitazamo yao.
Dkt Jingu amesema lengo la mafunzo hayo kwa wanataaluma ni kuboresha huduma za Afya kwa kuhakikisha wawezesha wanataaluma kuweza kujifunza njia mpya na za kisasa za kufanya kazi, ikiwemo kubaki na ujuzi na maarifa" amesema Dkt Jingu.
Mwenyekiti wa kamati ya mafunzo Endelevu ya kitaaluma (CPD) Remla Shirima amesema kwa mwaka 2021 Baraza lilianza utaratibu wa wanataaluma kuhuisha leseni zao kwa kutumia alama.
Mwenyekiti huyo amesema mwaka 2022 baraza lilitumia alama 5 za mafunzo endelevu katika kuhuisha leseni ambapo jumla ya wanataalama 18,132 waliweza kuhuisha leseni zao sawa na asilimia 71 ya wanataaluma wote waliokuwa wamesajiliwa.
Amesema mwaka 2023 Baraza lilitumia alama 10 za mafunzo katika kuhuisha leseni ambapo jumla ya wanataaluma 20,747 waliweza kuhuisha sawa na asilimia 62
"Mwaka 2024 Baraza lilitumia asilimia 20 na wanataaluma 15,887 waliweza kuhuisha leseni zao sawa na asilimia 42,"amesema Mwenyekiti huyo.
Amesema kumekuwa na namna mbalimbali ya kutatua changamoto hizo ikiwemo kamati kushiriki katika kutoa mada katika mikutano 15 na katika makongamano ya afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali,Prof. Tumaini Nagu amesema kazi yao kubwa ni kuinua ubora wa maisha hivyo kifo au ulemavu unapotokea kwa sababu ya uzembe tunakuwa hatujamtendea haki mgonjwa na hana sehemu ya kukata rufaa.
"Ni muhimu sana tukazingatia weledi na weledi unakuja kwa kujua ni tiba gani kwa wakati huo hivyo hatuna nafasi ya kufanya makosa ndio maana tunakazania suala la kujiendeleza," amesema Prof Nagu.
Mganga huyo wa Serikali amesema kwa sababu hiyo wanakazia mafunzo endelevu kwa wanataaluma.
Mwenyekiti wa MCT, Prof. David Ngassapa amesema mwitikio wa wanataaluma kujiunga na wataendelea kuwaelimisha ili kutoa huduma bora.
Mkutano huo umehudhuriwa na Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Wizara ya Afya, wasajili wa mabaraza mbalimbali, Mameneja wa programu mbalimbali, wajumbe wa MCT,Wawakilishi wa Association zinazotoa mafunzo endelevu, Wawakilishi wa Hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali za Mikoa, Wilaya, Wawakilishi kutoka katika Vyuo Vikuu,vya kati na NG'Os mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake