Friday, May 10, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AJUMUHIKA NA WANANCHI WA CHUINI KATIKA IBADA YA SALA YA IJUMAA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kudumisha, Umoja, Upendo na Mshikamano sambamba na kuitunza Amani na utulivu uliopo nchini kwa faida vya vizazi vijavyo.

Ameyasema hayo alipokuwa akiwasalimia waumini wa Dini ya kiislamu katika Masjid Mubaraka Chuini Wilaya ya Magharib “A” Unguja mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Alhajj Hemed amesema ili Taifa lipige hatua kimaendeleo ni lazima kuwepo na Amani na Utulivu ndani ya nchi, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuienzi na kuilinda Amani iliyopo nchini kwa faida ya vizazi vya sasa na baade pamoja na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa pili amesema waumini ni lazima kuitumia misikiti katika kujadili mambo mbali mbali yanayotokea katika jamii ikiwemo masuala ya utunzaji wa Amani na utulivu katika nchi na jamii tumazoishi, kwani kufanya hivyo ni kufuata nyayo za kiongozi wa kiislamu mtume Muhamad (S.A.W)

Amesema kuwa waumini wa dini ya kiislamu nilazima kufata mila ,silka na desturi walizokuwa nazo wanazuoni waliopita ili kupata radhi za Alaah (S.W) pamoja na kusoma historia na asili ya sehemu ili kuweza kuwarithisha vijana na kuweza kuwacha alama wakati wanapoondoka duniani.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed ameendelea kuwakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuendelea kuliombea duwa Taifa pamoja na viongozi waliopo madarakani ili waendelee kuwaongoza wananchi katika hali ya Amani na Utulivu utakaopelekea maendeleo endelevu nchini.

Mapema akitowa hutba ya sala ya Ijumaa, khatibu wa Masjid Mubarak Ustadh Adam Said Khamis amesema imekuwa na jambo la kawaida kwa wananchi kusambaza taarifa zisizothibitishwa uhalisia wake ambazo hupelekea Kuipotosha jamii jambo ambalo ni kinyume na mafundisho na miongozo ya dini ya kiislam.

Ustadh Adam amefahamisha kuwa uislamu umekemea vikali kusambaza jambo lisilothibitishwa na mamlaka husika ambalo linaweza kuichafua taswira ya mtu ama Taifa, hivyo amewataka wananchi kujenga tabia ya kupeana taarifa sahihi za matukio yanayotokea katika jamii ili kuepusha taharuki na migogoro inayoweza kujitokeza katika jamii zao.

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake