ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 24, 2024

SERIKALI KUONGEZA MADAKTARI BINGWA WA MOYO NA SARATANI


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Dr. Suzan Homeida kutoka Nchini Rwanda na Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Dr.Suzan Homeida kutoka Nchini Rwanda, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 23-5-2024 na (kulia kwa Rais) CEO wa PDB Prof.Mohamed Hafidh na (kushoto kwa Rais) Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Hassan Khamis Hafidh

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeeleza azma ya kuwekeza wataamu na madaktari bingwa kwenye hospitali mpya za wilaya na mikoa nchini ili kuwapunguzia gahamara kubwa wananchi wa Zanzibar wanaofuata matibabu nje ya nchi hasa kwa maradhi ya moyo, saratani, uti wa mgongo na ubongo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Daktari Suzan Homeida, raia wa Sudan anayefanyia kazi zake nchini Rwanda.

Dk. Mwinyi alimueleza daktari Homeida kwamba, Zanzibar inahitaji ushirikiano wa kina kwa madaktari bingwa na wataalamu kwa maeneo manne ya Afya ikiwemo wataalamu na madaktari bingwa wa Upasuaji wa Moyo, saratani, mfumo wa mishipa ya fahamu inayohusisha uti wa mgongo na ubongo.

Alisema, Serikali hutumia fedha nyingi na watu wanatumia gharama kubwa kufata huduma hizo nje ya Zanzibar hasa kwa nchi za India, Uturuki, Kenya na maeneo mengine duniani.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimweleza Dk. Suzan kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye kuongeza nguvu kwa hospitali ya Mkoa ya Lumumba ambayo inahitaji wataalamu wenye uweledi wa ubobezi wa hali ya juu kwenye maeneo hayo, nakuongeza liya ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vifaa vya kisasa kwenye hospitali hiyo bado inahitaji wataalamu wabobezi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimuomba Daktari huyo kuangalia pia, uwezekano wa kuwapata wataalamu na madaktari bingwa kutoka Sudan kwa vile anauzoefu nao wa muda mrefu hata wataalamu wa kawaida ili kuongeza nguvu kwenye hospitali za Wilaya za Unguja na Pemba kwa kuendelea kulisukuma gurudumu la afya Zanzibar kwenye uwekezaji mkubwa wa Sekta ya Afya nchini.

Naye, Daktari Suzan Homeida amepongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa hasa kwenye sekta ya Afya na kusifu hatua ya ujenzi wa hospitali za kisasa za Wilaya ya Mikoa zenye miundombinu na vifaa vya kisasa baada ya kuzitembelea akiongoza na timu ya uongozi wa Wizara ya Afya ukiongonzwa na Waziri mwenye dhamana, Nassor Ahmeid Mazrui.

Dk. Homeida ameiahidi Serikali kushirikiana nayo ili kuendeeza sekt ya Afya, Zanzibar.

Akizungumzia sekta ya Utalii wa Zanzibar, amesifu uzuri wa visiwa na fursa zilizomo zinazotokana na sekta hiyo akieleza matumaini yake makubwa kwa vivutio vya utalii akilenga zaidi utalii wa Afya kwa miaka ya baadae.

Aidha, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba anamengi ya kufanya kwa bara la Afrika, ikiwemo Zanzibar akiwa na ndoto ya kuanzisha Chuo kikubwa zaidi cha Afya, Dar es Saalam baada ya kile Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba na Teknolojia cha mjini Khartoum, Sudan.

Pia, alimueleza Rais Dk. Mwinyi uwezekano wa kuanzisha chuo cha Afya Zanzibar, kitakachofungua fursa nyingi na kuendeleza sekta ya Afya nchini hata kutoa ushirikiano wake kwa Serikali kupitia utaalamu wake wa udaktari.

Vilevile, Dk. Homeida alieleza, kuwepo kwake Zanzibar kutampatia uzoefu mpya wa kutengeneza mafanikio zaidi ya kukuza sekta ya Afya visiwani hapa hasa kwenye hospitali mpya za Wilaya.

Dkt. Suzan Homeida ni daktari mshauri mkuu wa magonjwa ya damu na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya “Frontierpoly21” iliyopo mjini Kigali, Rwanda pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba na Teknolojia mjini Khartoum, Sudan.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.

No comments: