ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 24, 2024

WAGOMBEA 14 WATEULIWA KUWANIA KITI CHA UBUNGE JIMBO LA KWAHANI


Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani, Bi. Safia Iddi Muhammad akibandika fomu za uteuzi za wagombea 14 kutoka vyama vya siasa vyenye usajili kamili walioteuliwa kuwania nafasi ya kiti cha Ubunge Jimbo la Kwahani. Uteuzi w wagombea hao ulifanyika leo tarehe 23 Mei, 2024.
Baadhi ya wanachama na wagombea wa Vyama mbalimbali vya siasa vilivyosimamisha wagombea katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kwahani Mkoa wa Mjini Magharibi, Zazibar wakikagua fomu za uteuzi za wagombea zilizobandikwa leo baada ya uteuzi.

Na Mwandishi wetu, Unguja
JUMLA ya wagombea 14 kutoka vyama vya siasa vyenye usajili kamili wameteuliwa kuwania kiti cha Ubunge katika Jimbo la Kwahani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani, Bi. Safia Iddi Muhammad leo tarehe 23 Mei, 2024 amesema Kati ya wagombea hao tisa ni wanawake na watano ni wanaume.
 
Bi. Safia amesema wagombea hao wote ni wale waliojitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha ndani ya muda uliopangwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Fomu za uteuzi kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo zilianza kutolewa kuanzia tarehe 17 hadi 23 Mei, 2024 ambayo pia ilikuwa siku ya uteuzi.
Bi. Safia amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi limekwenda vizuri na amevipongeza vyama vyote vilivyojitokeza kugombea nafasi hiyo.

"Zoezi la uteuzi wa wagombea katika Jimbo la Kwahani limekwenda vizuri na tayari majina ya wagombea 14 waliojitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha wameteuliwa kuwania kiti hicho," alisema Bi. Safia.

Msimamizi huyo wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani, amewataja wagombea walioteuliwa na Vyama vyao katika Mabano kuwa ni Bw. Bashir Yatabu Said (Demokrasia Makaini), Bi. Nuru Abdulla Shamte (DP), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan (NLD), Bi. Zainab Maulid Abdallah (CCK), Bi. Tatu Omary Mungi (UPDP), Bw. Khamis Yussuuf Mussa (CCM) na Bi. Jarade Ased Khamis (AAFP).

Wengine amewataja kuwa ni Bw. Kombo Ali Juma (NRA), Bi. Shara Amran Khamis (ADC), Bi. Naima Salum Hamad (UDP), Bi. Madina Mwalim Hamad (ADA TADEA), Bw. Amour Haji Ali (SAU), Bi. Mashavu Alawi Haji (UMD) na Bw. Abdi Khamis Ramadhan (CUF).
 
Bi. Safia amesema tayari ameshakutana na wagombea wa Vyama vyote na wapo tayari kuanza kampeni.

Kwa mujibu wa Taarifa ya INEC iliyotolewa kwa umma na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Bw. Kailima, R. K jijini Dodoma tarehe 02 Mei, 2024 kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zitafanyika kuanzia tarehe 24 Mei, 2024 hadi tarehe 07 Juni, 2024 na uchaguzi utafanyika tarehe 08 Juni, 2024.

No comments: