Advertisements

Sunday, May 19, 2024

WIZARA YA MADINI, WAFANYABIASHARA WA BARUTI WAJADILI CHANGAMOTO


Kamishna wa Madini Dk Abdulrahman Mwanga ameongoza kikao kazi cha wataalam wa Wizara, Tume ya Madini na wawakilishi wa Umoja Wafanyabiashara wa Baruti Tanzania (TEDA) kilicholenga kujadili changamoto zinazohusiana na biashara ya baruti nchini.

Kikao hicho kilichofanyika leo Mei 18, 2024 katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma, kimetumika kupokea changamoto, maoni, mapendekezo na ushauri kutoka kwa Umoja huo ambapo pia Wizara imekitumia kujibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa huku nyingine zikipokelewa kwa ajili ya kuendelea kufanyiwa kazi.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk Mwanga ameupongeza Umoja huo kwa kuona umuhimu wa kukutana na Wizara ili kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali yanayohusu biashara ya baruti nchini na kueleza kuwa, vikao kama hivyo vitasaidia kujenga mahusiano mazuri ikiwemo kubaini mapungufu na changamoto katika utekelezaji wa Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali zinazosimamia biashara ya baruti.

" Sote tunafahamu bila biashara ya baruti hakuna uchimbaji, ninawapongeza kwa kuona umuhimu wa kukutana na sisi kujadili kwa pamoja changamoto zenu na nina amini vikao hivi vitakuwa chachu ya kufanya maboresho yanayofaa kwa Maendeleo ya Sekta hii," amesema Dkt. Mwanga.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TEDA Mhandisi Gideon Kasege akizungumza katika kikao hicho ameipongeza Serikali kwa kuandaa Kanuni za Baruti ambazo zimeruhusu wauzaji wengi ikiwemo usafirishaji wa baruti.

Pamoja na hayo, Mhandisi Kasege ametoa angalizo kwa Serikali kuendelea na udhibiti wa biashara hiyo ambayo inaelezwa kuwa miongoni mwa bidhaa hatarishi.
Pamoja na masuala mengine yaliyowasilishwa, umoja huo umetoa ombi kwa Wizara la kuwa na mfumo wa vibali vya baruti kwa njia ya mtandao ili kuondoa changamoto za upatikanaji wake.

Wizara ya Madini imekuwa na utaratibu wa kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokabili kila makundi ikiwemo wachimbaji wakubwa na wa kati, wachimbaji wadogo wa madini ya aina mbalimbali, watoa huduma migodini na wafanyabiashara wa madini kwa lengo la kujadili changamoto, kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kwa lengo la kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.
Kikao hicho kimeazimia kukutana kila robo mwaka.

Jukumu la utoaji wa leseni ya biashara ya baruti ni moja ya shughuli zinazofanywa na Wizara ya Madini Makao Makuu.

No comments: