ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 18, 2024

TUME YA USHINDANI YATAKA UBORA WA BIDHAA,YATOA RAI KWA WATANZANIA


TUME ya Ushindani (FCC) imewahakikishia wawekezaji kutoka nje ya nchi wanaokuja nchini Tanzania kuwekeza kwani kuna mazingira salama ya uwekezaji pamoja na kufanyabiashara.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Wiki ya Kudhibiti bidhaa bandia duniani ambayo huadhimishwa kati ya Juni na Julai ya kila.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikihimiza wawekezaji kutoka nje kuja nchini ili kufanya uwekezaji pamoja na biashara sambamba na kudhibiti ubora.

Kuhusu ubora wa bidhaa ,Erio amewashauri wananchi kuacha mara moja matumizi ya bidhaa bandia na badala yake wanunue na kutumia bidhaa halisi ili kusaidia kuchochea uwekezaji, kukuza fursa za ajira na hatimaye kuchagiza ukuaji wa uchumi wao na taifa kwa ujumla.

“Tusikubali kununua bidhaa bandia na hii itasaidia hata wale wanaokuja kuwekeza watakapofanya tathimini ya bidhaa zilizopo wakute tunatumia bidhaa halisi na zilizobora."

Pia amesema kati ya asilimia 2.5 na 3.5 ya biashara zinayofanyika ulimwenguni zinahusisha bidhaa bandia huku akibainisha baadhi ya madhara ya bidhaa hizo kuwa ni kutopata thamani halisi ya fedha pamoja na madhara mbalimbali ya kiafya kwa watumiaji

Akizungumzia Wiki ya kudhibiti bidhaa bandia duniani amesema wiki hiyo inaadhimishwa sehemu zote duniani kati ya Juni na Julai na sababu yake ni kwamba bidhaa bandia zina changamoto nyingi.

Ametaja baadhi ya athari za bidhaa bandia kuzorotesha biashara, uchumi na kukosena kwa ajira nchini."Bidhaa bandia zina matatizo hata katika maeneo ya kiuchumi kwanza zinaathiri ubunifu kwasababu katika kushindana unatakiwa kila kitu uje na kitu kipya kuwa na bidhaa katika uchumi kunadhorotesha biashara.

Katika maadhimisho ya mwaka huu kauli mbiu inasema Kudumisha uhalisia kwa kulinda ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi nchini na inatarajiwa kuadhimishwa Julai 18 katika ukumbi wa mikutano ya Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Pia katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho mbalimbali ya wajasiriamali na wamiliki wa viwanda vidogovidogo pamoja na majadiliano ya jopo.

No comments: