ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 7, 2024

Balozi wa Sweeden nchini afanya ziara mkoani Manyara.



Na John Walter -Babati
Balozi wa Sweden nchini Tanzania Bi Charlotte Ozaki hii leo agosti 7,2024 amefanya ziara ya kutembelea Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Manyara ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu iliyoanzia mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na hatimaye kutamatika ndani ya mkoa wa Manyara.

Katika ziara hiyo Balozi Bi Charlotte amepata wasaa wa kukutana na uongozi pamoja na wanachama wa klabu hiyo na kujadili mambo mbalimbali muhimu kwaajili ya maendeleo ya tasnia ya habari mkoani Manyara ikiwemo fursa zilizopo lakini pia changamoto zinazowakabili waandishi mkoani humo.

Zacharia Mtigandi, mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Manyara ameomba Chama kipatiwe mafunzo ya namna Bora ya uandishi wa maandiko ya miradi ili iweze kukisaidia chama kifedha kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuwezesha shughuli za chama zifanyike kwa ufanisi zaidi.

"Kutokana na changamoto za kifedha tunatamani UTPC pamoja na ubalozi wa Sweden hapa nchini ambao ni wadau wetu muhimu watupatie mafunzo ya namna bora ya kuandika maandiko ya miradi ili tuweze kupata fedha zitakazosaidia kuendesha shughuli za chama chetu" alisema Mtigandi

Mzidalifa Zaidi, mwandishi wa habari mkoani Manyara alitoa baadhi ya kero ambazo wanapitia kama waandishi wa habari wanawake katika utendaji wa shughuli zao ikiwemo kutishiwa kubakwa hali inayofanya kuwa na hofu pale wanapotekeleza majukumu yao.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na afisa ustawi kutoka dawati la jinsia lililopo chini ya jeshi la polisi mkoani Manyara ndugu Kurwa Mahige ambaye ameshauri serikali kujenga nyumba za akiba zitakazotumika kuwahifadhi waathirika wa matukio ya ukatili ili kusaidia mahakama ifanye kazi yake vizuri lakini pia kuhakikisha ulinzi na usalama wa waandishi wanapotekeleza majukumu yao.

Akizungumza baada ya kusikiliza Hoja mbalimbali, Balozi Charlotte amesema amefurahishwa kwa namna ambavyo Klabu ya waandishi wa habari mkoani humo kinavyofanya shughuli zake na namna waandishi wanavyoibua matukio na kusisitiza waongeze juhudi zaidi na kujipanga katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa ili kuripoti taarifa zitakazo kuwa na maslahi mapana kwa jamii bila kuleta taswira mbaya.

"Nimefurahishwa sana na kazi ambazo chama hiki kinafanya kwani ni tofauti kabisa na vyama vingine kwani lengo letu ni kutembelea na kuona namna vyama hivi 28 vilivyopo Tanzania vinavyofanya kazi, lakini nimependa zaidi namna jeshi la polisi linavyoshirikiana na waandishi wa habari katika kulinda usalama wao" alisema Balozi Charlotte

Aidha Balozi Charlotte ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa zaidi kupitia muungano wa vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC) kwa lengo la kuendelea kuwashika mkono na kuwasaidia kwa mambo mbalimbali kwa kuwa wao ni wafadhili wakuu wa muungano huo.

Kwa sasa ni takribani miaka 61 tangu nchi ya Sweden kufadhili waandishi wa habari hapa nchini Tanzania kupitia muungano wao na tayari mambo mengi yamefanyika ikiwemo kutoa mafunzo kwa waandishi juu ya mambo tofauti tofauti yahusuyo tasnia hiyo lakini pia kuwasaidia kifedha ili kuwawezesha kuajiri wataalamu katika ofisi zao na kununua samani za ofisi.

No comments: