Kanisa Katoliki Tanzania limetoa muongozo mpya kuhusu shughuli za ki imani zikihusisha utaratibu wa ibada na salamu za rambirambi katika misa ya miziko.
Taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Liturujia Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Stefano Kaombe likirejea kikao kilichoongozwa na Askofu Mkuu Jude Thadeus Ruwa’ichi imesema utaratibu wa salamu hizo kwa sasa utahusu wawakilishi watano pekee.
Wawakilishi hao ni Mmoja kutoka parokia, Jumuiya, Chama chake cha Kitume, Ajira na Kiongozi wa jamii (mtendaji, diwani).
Pd. Kaombe amesema katika mkutano wa Waklero wote ulioanyika Juni 25, 2024, katika Kituo cha Msimbazi, mkutano ulielekeza kuwa kabla ya komunyo katika tukio la msiba maelekezo yatolewe kwa kuzingatia kuwa wanajumuika waamini wa madhehebu na imani mbali mbali.
“Sasa tunaingia hatua ya kupokea Ekaristi Takatifu. Hili ni tendo la pekee la kiimani. Wanaalikwa kushiriki Wakristo Wakatoliki waliojiandaa kiroho ipasavyo,” ilisema taarifa ya Pd. Kaombe.
Amefafanua kuwa salamu za rambirambi katika Misa ya maziko zitolewe na wawakilishi tu zikifuatiwa na neno la shukrani toka katika familia.
“Rambirambi zingine zaweza kutolewa nyumbani na makaburini baada ya ibada,” imesema taarifa hiyo.
Vile vile Kanisa limesema Ibada ya marehemu katika Misa ina sehemu nne: nyumbani, mlangoni, Misa inaendelea bila ibada ya toba, sala ya buriani. Misa inahitimishwa bila baraka kanisani, kwani makaburini kuna maziko na Baraka ya mwisho.
Kuhusu Jeneza, taarifa hiyo imesema litengenezwe kwa namna nzuri, liweze kufunuliwa kutoka kushoto kuelekea kulia kwa marehemu, kama kuna sababu za msingi si lazima kufungua jeneza wakati wa sala ya buriani.
Aidha wakati wa kunyunyizia maji ya Baraka na kufukiza ubani, ni kipindi cha ukimya na maombolezi ya moyoni, hakuna sala ya hadhara katika maombezi kwa marehemu wetu.
No comments:
Post a Comment