Tuesday, September 10, 2024

DKT.DIMWA: ATAJA MAMBO MATANO YA KUUNGWA MKONO UONGOZI WA DK.MWINYI


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akiwahutubia,mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla katika mkutano wa hadhara uwanja wa Polisi Jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba.
BAADHI ya wanachama wapya wa CCM waliotoka ACT-Wazalendo, wakionyesha kadi za chama walichotoka wakati wakipokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dkt.Mohamed Said Dimwa, kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Polisi Kodende Mkoa wa Kaskazini Pemba.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,ameyataja mambo matano ya kujivunia na kuungwa mkono katika uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Mwinyi toka aingie madarakani.

Amefafanua kuwa mambo hayo ni Zanzibar yenye neema kwa wote kila mmoja anaiona, yajayo yametimia,Zanzibar salama yenye maendeleo endelevu imeanza kuonekana.

Aliyataja mambo mengine kuwa ni Zanzibar yenye kuheshimu,kulinda na kuenzi misingi ya demokrasia na siasa za maendeleo,Zanzibar yenye kuenzi na kulinda historia yake hasa ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Hayo ameyasema wakati akiwahutubia wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla wa Wilaya ya Micheweni huko katika mkutano wa hadhara wa uwanja wa Polisi katika jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba katika mwendelezo wa ziara ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar kisiwani Pemba.

Dkt.Dimwa, amesema dhamira ya Chama cha Mapinduzi ni kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi unaotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili wananchi wa makundi yote wanufaike na fursa ya maendeleo endelevu.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa,alieleza kuwa Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja za kiuchumi,kijamii na kisiasa.

Alisema siri ya mafanikio hayo ni uwazi na uhuru uliowekwa na serikali kwa kufungua milango ya uwekezaji sambamba na kuweka sera na sheria rafiki katika uendeshaji wa biashara huria kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Tumejipanga vizuri kuiweka Zanzibar katika nchi za visiwa zilizoendelea kiuchumi na kwa kasi hii ya Rais Dk.Mwinyi ndani ya kipindi kifupi baada ya kukamilika kwa miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege vya kisiasa basi tujipange kwa sote kuvuna matunda ya serikali yenu.

Mapinduzi ya kisiasa yalifanyika mwaka 1964 tukajitawala na kuanza mikakati ya kujenga nchi sasa tupo katika awamu nyingine ya kufanya Mapinduzi ya kiuchumi na kimaendeleo ili vizazi vijavyo waishi maaisha yenye hadhi na yaliyo bora zaidi”, alisema DkT.Dimwa.

Kupitia mkutano huo, aliwasihi wananchi wa kisiwa cha Pemba kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi ili waweze kunufaika na siasa zisizokuwa na ubaguzi wa rangi,dini,ukanda na ukabila.

Alisisitiza wananchi wa kisiwani humo kupuuza kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa ACT-Wazalendo kwani wengi wao tayari wanaona kasi ya maendeleo imekuwa kubwa hivyo wanapotosha na kubeza Serikali ili kutafuta huruma kwa wananchi waliowasaliti kupitia ahadi zao zisizotekelezeka.

Kupitia mkutano huo, zaidi ya wanachama 150 kutoka chama cha ACT-Wazalendo na CUF wamejiunga na CCM ili kupata uhuru wa kisiasa unaotokana misingi ya haki na demokrasia iliyopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Wanachama hao wapya wameeleza kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakipotoshwa na kupandimizwa siasa za chuki dhidi ya Serikali na CCM na kwamba wamebaini wenyewe nia ya dhati ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa na wakaamua kujiunga na CCM kwa hiari yao.

No comments: