Wednesday, September 25, 2024

ONGEZEKO LA MARADHI YASIYOAMBUKIZA NI TISHIO ZANZIBAR


Katibu wa Muungano wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza (NCDA) Omar Abdalla Ali akitoa mafunzo yanayohusu maradhi yasioambukiza na vichocheo vya maradhi hayo kwa Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali na Wasanii huko katika Ukumbi wa Uzazi salama Kidongo Chekundu

Na Khadija Khamis 
Katibu wa Muungano wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza Omar Abdalla Ali amesema ukosefu wa mlo kamili katika jamii ni kichocheo kikubwa cha Maradhi yasioambukiza nchini.

Kauli hiyo ameitoa katika ukumbi wa uzazi salama huko Kidongo Chekundu wakati wa mafunzo ya waandishi wa Habari na wasanii amesema takriban Maradhi mengi yasiyoambukiza hutokana na mfumo duni wa ulaji jambo ambalo linachangia ongezeko kubwa la maradhi hayo.

“ Jamii bado haina Utamaduni wa kutumia mbogamboga na matunda bali hutumia uwanga na mafuta kwa kiasi kikubwa ni kichocheo cha maradhi hayo,”amesema Katibu Omari.

Ameeleza kuwa Maradhi yasiombukiza yanavichocheo vingi ambavyo Jamii inapaswa kuviepuka kama matumizi ya sigara, pombe, kuwa na uzito wa kupitiliza, pamoja na msongo wa mawazo .

Aidha amesema tafiti zinaonyesha kuwa shindikizo la damu na Maradhi ya kiharusi huongoza kusabisha vifo ingawa Jamii bado haijakuwa na hofu juu ya ongezeko hilo ambalo linapunguza nguvu kazi ya taifa. .

Hata hivyo ameitaka jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara njia ambayo itasaidia kujua afya zao, katika wakati sahihi iwapo wameonekana na viashiria vya maradhi hayo kwa hatua za awali kutasaidia kupatiwa matibabu ya haraka.

Naye Mkufunzi Mwandishi Muandamizi Suleiman Seif Omar amewataka waandishi wa Habari kutumia njia sahihi ya kupeleka ujumbe kwa jamii ili kupata hamasa ya kujilinda na vichocheo pamoja na kufuata maelekezo na ushauri kwa wataalamu wa afya

Kwa Upande wa Meneja wa Muungano wa Jumuiya ya Maradhi yasiombukiza Haji Khamis Fundi amesema hutokana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa wagonjwa wanaoishi na maradhi hayo iko haja kwa jamii pamoja na familia kiujumla kuwatizama kwa jicho la kuwapa matumaini sio vyema kuwatelekeza wazee wao .

Alifahamisha kuwa Serikali inapata mzigo Mkubwa kutokana na gharama kubwa za dawa za maradhi hayo pamoja na ongezeko la wagonjwa jambo ambalo linaadhiri uchumi wa nchi.

“Sera na Mikakati maalumu inahitajika kwa kuiunga mkono serikali kwa kuengeza mashirikiano kwa wafadhili mbali mbali wa ndani na nje ya nchi ili kupambana na maradhi hayo.”amesema Meneja wa NCDA

Kwa Upande wa washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo Kwa kutoa elimu Kwa jamii ya kuepukana na vichocheo vya maradhi hayo pamoja kuwapa hamasa ya kupima Afya zao.

Asilimia 80 ya wagonjwa wa maradhi hayo hugundulika katika hatua ya tatu na ya nne kwa Zanzibar jambo ambalo husababisha matibabu yake kuwa magumu.

No comments: