Thursday, September 5, 2024

USAFI WA MAZINGIRA UWE SHIRIKISHI KWA JAMII - DC MPOGOLO


Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuimarisha usafi wa mazingira katika eneo la Buguruni kisiwani.

Mhe.Mpogolo ameyasema hayo katika ziara yake ya kutembelea na kukagua mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka majumbani eneo la Buguruni kisiwani.

"Niwaagize DAWASA ndani ya wiki mbili kupitia upya mradi huu na kumaliza changamoto zilizobainika na kusababisha Mazingira ya Buguruni kuwa katika ya kutoridhisha, lakini zaidi niwaombe wananchi kuwa na matumizi sahihi ya miundombinu hii ya majitaka na wao kutokua sababu yakufanya izibe mara kwa mara" alisema Mhe. Mpogolo
Naye ameongeza kuwa Serikali ilitekeleza mradi huu kwa nia njema ya kuwasaidia wananchi wa maeneo haya kukabiliana na gharama kubwa za uondoshaji majitaka zilizowakabili awali, lakini pia kuboresha usafi wa mazingira kwa kumaliza changamoto za utiririshaji majitaka mitaani.

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo Charles Makoye ameeleza kuwa Mamlaka inampango wa kufanya maboresho katika mradi huo lakini zaidi kuwa na timu maalumu itakayofuatilia mradi kwa karibu kila siku.
"Pamoja na maboresho tutakayoenda kufanya niwaombe wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hii ili tatizo la uzibaji lisitokee mara kwa mara na majitaka kusambaa mitaani kwani changamoto kubwa ya mradi wetu huu ni matumizi yasiyo sahihi kutoka kwa wananchi"ameeleza Makoye.

Bi Aisha Ally mkazi wa Buguruni kisiwani ameshukuru Serikali kwa kufika na kusikiliza changamoto ya utiririkaji majitaka mitaani waliyokua nayo huku akiwa na imani DAWASA watatatua changamoto hiyo kwa wakati ndani ya wiki mbili.

No comments: