RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaahidi Wazanzibari kuibadili Zanzibar kuwa kituo bora cha biashara cha kimataifa kwa kutoa fursa za mwingiliano wa wafanyabiasha kutoka mataifa mbalimbali ya dunia kuja nchini, kuuza na kununua.
Amesema hatua hiyo inakuja kwa kuweka miundombinu imara ya masoko ya kisasa yatakayotoa huduma za biashara kwa saa 24 za siku pamoja na kuimarisha miundombinu ya kisasa ya barabara kubwa na kutanua viwanja vya ndege vyenye hadhi ya kimataifa Unguja na Pemba vitakavyoruhusu kutua ndege kubwa za kimataifa za safari za moja kwa moja.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua soko jipya la ghorofa mbili Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayoiongoza.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kuunganisha huduma rahisi ya usafiri wa Umma kwa kuagiza mamlaka zinazosimamia masoko kujenga vituo vikubwa vya mabasi vitakavyoruhusu muingiliano wa moja kwa moja baina ya masoko hayo ya Kwereke, Jumbi na Chuini ili kutoa fursa kwa wananchi na wafanyabiasha kunufaika na neema za masoko hayo.
Akizungumzia mwenekano mpya wa haiba ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kufanya mageuzi makubwa ya kubadili mandhari mpya ya miji ya Zanzibar ndani ya mwaka mmoja ujao wa uongozi wake kwa kujenga madaraja mawili makubwa kwa mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja ili kuruhusu mwingiliano rahisi wa mikoa hiyo kibiashara na Utalii kwa kujenga barabara za juu kutoka Uzi Ng’ambwa Kaskazini Unguja hadi Charawe – Chwaka mkoa wa Kusini Unguja ili kurahisiaha sekta ya usafiri na usafirishaji kwa mikoa hiyo.
Dk. Mwinyi amesema, wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na mageuzi makubwa hasa kwa viwanja vya ndege vya Abeid Amani Karume na Uwanja wa ndege wa Pemba kwa kuahidi kuifanyia matengenezo makubwa “Terminal 2” kuwa na hadhi ya kimataifa pamoja na kutoa kituo kikubwa cha biashara kwa eneo hilo litakalo kuwa la kwanza kwa uzuri na ubora Afrika Mashariki na kujenga upya uwanja wa ndege wa Pemba kuwa wa Kimataifa.
Akizungumzia bandari Jumuishi ya Maghapwani inayotarajiwa kuwa kichochezi kikubwa na kukuza biashara nchini, Rais Dk. Mwinyi amesema tayari fedha ya ujenzi wa bandari hiyo zimekamilika na hatua zote za kuanza kwa ujenzi huo ziko tayari.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi ameziagiza mamlaka zinazosoimamia Soko la Mwanakwerekwe kutowatoza ushuru mkubwa wafanyabiashara wa eneo hilo na kueleza fedha zilizojengewa soko hilo sio mkopo bali kodi za wananchi wenyewe hivyo Serikali haitegemei chochote kutoka kwa wananchi na wafanyabishara wa soko hilo isipokua fedha hizo zitasaidia kuliendesha soko hilo kwa kulitunza.
Pia, Dk. Mwinyi amewaagiza wanaosimamia soko hilo la Kwerekwe kusimamia utaratibu wa wafanyabiashara hao kwa kuwazuia wasifanye biashara kwenye hifadhi ya biashara na maeneo yasiyo rasmi na kuwasihi waendelee kulisimamia kwa weledi na kulitunza soko hilo.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwaahidi wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali sokoni hapo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaongezea mitaji ya biashara zao endapo wanakuwa na utaratibu mzuri wa kujiweka kwa makundi ili kupata mikopo.
Naye, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameeleza kazi ya kubuni na kutekeleza maendeleo sio ya viongozi pekee bali ni ya watu wote, hivyo amewataka Wananchi kuungamkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya za kuwaletea maendeleo. Hata hivyo amesema kufunguliwa soko la Kwerekwe kutatoa zaidi ya ajira laki moja na na kuwanufaisha watu wengi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Muhamed Mchengerwa, akizungumza kwenye ufunguzi wa soko hilo, amesifia michango ya Viongozi wakuu wa nchi Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Mwinyi wanavyofanya makubwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadae kama ilivyokua kwa waasisi wa taifa hili, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na baba wa Taifa, Julius Kambarage Nuyerere.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed amempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uamuzi wa kuekeza mradi mkubwa wa soko la Mwanakwerekwe na kusifu mafaniko makubwa ya kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo.
Ujenzi wa soko la Mwanakwerekwe lenye uwezo wa kuwahudumia wafanyabiashara zaidi ya 5,000 kwa wakati mmoja watakaowekwa kwa mpangolio utakaoendana na hadhi ya soko hilo kwa kila mmoja kuhakikishiwa kutimiza mahitaji yake ya kuwafikia wateja wake, umegharimu shilingi bilioni 35.8
Soko hilo litawajumuisha wafanyabiashara wa wanafaka, mama na babalishe, wauza samaki, kuku, nyama, mbogamboga, chini ya uangalizi wa usalama wa kamera za CCTV.
Aidha, soko hilo limejengwa mkandarasi Jeshi la Kujenga Uchumi, JKU chini ya usimamizi na ushauri wa timu ya wahandisi wazalendo limejumuisha sehemu za kuhifadhia magari zaidi ya 120 ya watakaoingia na kutoka sokoni hapo, kuna ghala 15 yatakayo ruhusu magari ya moja kwa moja kushusha bidhaa eneo hilo, vyoo vyakidhi mahitaji ya soko hilo, jiko maalumu kwa wajasiriamali na mamalishe, chumba maalum cha baridi kwa wafanyabiashara wenye mahitaji hayo, chumba Maalumu ya kunyonyeshea watoto, sehemu za minada, machinjio ya kuku, umeme wa uhakika wa jenereta maalumu la dharura na maji ya uhakika.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment