ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 31, 2024

SERIKALI NA TAASISI BINAFSI ZINATUMIA KUMBUKUMBU NA NYARAKA KATIKA KUPANGA, KUTATHMINI NA KUFANYA MAAMUZI KWA AJILI YA UTEKELEZAJI


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa utunzaji nzuri wa kumbukumbu na Nyaraka unapelekea kwa kiasi kikubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji nchini.

Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussen Ali Mwinyi katika Mkutano wa kumi na mbili(12) wa Chama cha Menejiment ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Amesema kuwa Serikali na Taasisi binafsi zinatumia kumbukumbu na Nyaraka katika kupanga, kutathmini na kufanya maamuzi kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi au Taasisi husika.

Makamu wa Pili wa Rais amesema utunzaji mzuri wa kumbukumbu na nyaraka unachangia kuboresha vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato kupitia taarifa zilizohifadhiwa zinasaidia kuonesha maeneo ya uwekezaji yakiwemo ya utalii yanayokuza pato la Taifa na kuimarisha miradi ya maendeleo.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa kumbukumbu na nyaraka zinaisaidia Serikali katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma na kutumika kama nyezo muhimu inayomsaidia Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kukagua na kudhibiti uhalali wa matumizi ya fedha za Umma.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amesema kumbukumbu na Nyaraka zinaisaidia Serikali kufahamu taarifa za watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo, wanaotarajiwa kustaafu pamoja na mambo mengine ikiwemo haki na wajibu kwa wafanyakazi.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amezitaka Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri wa kukutana na Uongozi wa TRAMPA ili kuangalia changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa watendaji wa kada hio na kuzichukulia hatua stahiki kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji wao.

Aidha Amewataka wataalamu wa kada ya Kumbukumbu na Nyaraka kufanya kazi kwa kufuata miiko na maadili ya kazi zao pamona na kutunza siri ili kulinda heshima ya taaluma hio kwa maslahi mapana ya Taifa.

Nao Mawaziri wenye dhamana ya Wizara ya Utumishi kutoka SMT na SMZ Mhe. GEORGE BONIFACE SIMBACHAWENE na Mhe. HAROUN ALI SULEIMAN wamesema watunza kumbukumbu na Nyaraka wana wajibu wa kukuza na kutunza uadilifu katika misingi ya utumishi wa Umma wakati wote wanapokuwa katika majuku yao.

Wamesema kuwa kwa kuona umuhimu wa watunza kumbukumbu na nyaraka katika Taasisi zote nchini, Serikali imejipanga kuajiri watumishi zaidi ya 1056 ambao wataongeza nguvu ya utendajikazi katika kada hio na kuleta tija katika kuwatumikia Watanzania.

Aidha wamesema wizara zitahakikisha zinazingatia maslahi ya watumishi wote wakiwemo wa kada hio sambamba na kuwapatia mafunzo na ruhusa za kushiriki katika mikutano mbali mbali inayowajengea uwezo na maarifa ya kufanya kazi zao kwa uweledi na ufanisi mkubwa, hivyo wametoa wito kwa viongozi wa taasisi za serikali na zisizo za serikali kuhakikisha wanazifanyia kazi changamoto zinazoikabili kada hio katika taasisi zao kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Taifa.

Akisoma risala ya wanachama wa chama hicho Mwenyekiti wa Chama cha Menejiment ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania ( TRAMPA ) Bi. DEVOTHA GEORGE MROPE amesema chama kinatambua michango na Juhudi zinazofanywa na wanataaluna wa kada hio katika kuhakikisha wanazitunza vizuri Nyaraka na Kumbukumbu za Serikali na Taasisi binafsi kwa maendeleo bora uwekezaji na kukuza uchumi wa ya Taifa.

MROPE amesema kuwa Kumbukumbu na nyaraka zinapotunzwa vizuri zinaisaidia jamii na Serikali kutambua tulikotoka, tulipo na tunakoelekea hivyo TRAMPA imejipanga katika kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwapa taaluma na ujuzi watendaji wa kada hio ili kuongeza ari na ufanisi wa kazi zao.

Aidha amezipongeza Serikali zote mbili kwa kuanzisha matumizi ya Mifumo ya Tehama katika Taasisi za Serikali itakayosaidia kutunza Kumbukumbu kwa ufasaha na uweledi wa hali ya juu jambo ambalo litachangia kasi ya maendeleo nchini.

Mrope amesema changamoto kubwa inayoikabili TRAMPA ni waajiri kuendelea kutumia karatasi katika utunzaji wa kumbukumbu na Nyaraka pamoja na uhaba wa vyumba maalum kwa ajili ya masjala za siri jambo ambalo linachangia kwa kiasi mkubwa uvujaji wa taarifa siri katika Taasisi nyingi nchini, hivyo ameziomba serikali zote mbili kuweza kuzitatua changamoto hizo ili kuleta ufanisi nzuri wa kazi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR)Leo tarehe 30 / 10 / 2024.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi mbali mbali wa SMT na SMZ, washiriki na wadau waliohudhuria katika Mkutano wa kumi na mbili(12) wa Chama cha Menejiment ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussen Ali Mwinyi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

No comments: