ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 8, 2024

MAKATIBU WAKUU EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA TANZANIA YAENDELEA KUAMINIWA KUONGOZA MIKUTANO YA JUMUIYA


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi akiongoza Mkutano wa 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya makatibu wakuu uliofanyika tarehe 7 Novemba 2024.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango unaofanyika jijini Arusha.

Makatibu Wakuu wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo tarehe 7 Novemba 2024 jijini Arusha, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango unaotarajiwa kufanyika jijini humo tarehe 8 Novemba 2024.

Mkutano huo wa Makatibu Wakuu umepitia na kupitisha agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 34 wa Baraza la Mawaziri, baada ya kupokea taarifa iliyowasilishwa kwao na Wataalamu waliokutana tarehe 4 - 6 Novemba 2024.

Taarifa ya Wataalamu iliyowasilishwa imeelezea hali na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya na masuala mbalimbali yaliyokubaliwa katika mikutano iliyopita.

Masuala hayo ni pamoja na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ikijumuisha taarifa ya uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha, Taarifa ya Utekelezaji wa Utatu wa Pamoja wa COMESA-EAC-SADC, Mapendekezo ya Vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya Jumuiya kwa mwaka wa Fedha 2025/2026, Mapitio ya Utekelezaji wa Mkakati wa Sita (6) wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2021/2022- 2025/26) na Taarifa ya Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi ambaye aliteuliwa na Jamhuri ya Sudani Kusini kuongoza mkutano huo muhimu kwa niaba yao.

No comments: