Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amewataka Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha matamasha ya Utamaduni yanayofanyika katika maeneo yao yanafanikiwa na kuleta ushawishi na ushirikiano nchini kutoka kabila moja hadi lingine.
Akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga, kuhusu mkakati wa kuongeza thamani ya zawadi kwenye Tamasha la Utamaduni, Novemba 5, 2024 Bungeni jijini Dodoma, Mhe. Mwinjuma ameeleza kuwa, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha matamasha hayo ikiwemo kuandaa mipango ya kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi kupata ufadhili zaidi na kuboresha zawadi za tamasha lijalo.
Mhe. Mwinjuma alifafanua kwamba, chini ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Serikali imeamua kuyaunganisha makabila yote nchini na kuwa na tamasha moja la kitaifa. "Utaratibu wa tamasha hilo unafanyika kwa ushirikiano na OR - TAMISEMI na mkoa mwenyeji wa tamasha kwa mwaka husika," amesisitiza.
Aidha, amefafanua kuhusu maboresho ya zawadi, akisema kwamba kwa tamasha la mwaka 2024, washindi wa kwanza katika mashindano hayo walipata zawadi ya fedha taslimu ya shilingi milioni moja, ikilinganishwa na shilingi laki moja na nusu zilizotolewa hapo awali.
No comments:
Post a Comment