Wednesday, November 6, 2024

MLELE KUANZA KUTUMIA SHERIA NDOGO KUWABANA WATUPA TAKA HOVYO!

Na Zillipa Joseph, Katavi

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mlele mkoani Katavi wameridhia kuanza kutumika kwa sheria ndogo za Halmashauri hiyo hasa kwa watu wasiozingatia suala la usafi katika maeneo yao ya makazi na biashara.

Azimio hilo limekuja kwa lengo la kudhibiti uchafu katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo bwana Sudi Mbogo ametangaza uamuzi huo katika kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/ 2025 ambapo alisema watu wamekuwa na tabia ya kutupa taka hadi ndani ya mitaro na kusababisha mitaro kuziba.

Sheria hiyo ndogo ya usafi wa mazingira katika halmashauri ya Mlele itamwajibisha kwa kulipa faini ya shilingi elfu hamsini mtu yeyote atakayebainika kuchafua mazingira.

Bwana Mbogo ameeleza kuwa licha ya elimu juu ya usafi kutolewa bado wananchi wamekuwa wakikaidi na kutupa taka hovyo.

“Kamati ya fedha, uongozi na mipango iliridhia menejiment kutumia Sheria ndogo ili kuwabana wakorofi wachache ili kuweka mji wetu wa Inyonga kwenye mazingira ya usafi” alisema.

William Lula ni diwani katika halmashauri ya Mlele, alisema madhara ya uchafu ni pamoja na kusababisha magonjwa ya milipuko katika jami.

Aliongeza kuwa magonjwa .hayo yatasababisha serikali kutumia fedha nyingi kutibu watu watakaokuwa wameugua.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ilunde Martin Mgoloka alisema fmpango huo utasaidia kununua vitendea kazi vya usafi kutokana na edha zitakazopatikana katika faini hizo.

Baadhi ya wafanyabiashara wa Inyonga walipoulizwa kuhusiana na suala la usafi na kuanza kutumika kwa sheria ndogo waliunga mkono suala Hilo na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo mji wa Inyonga utakuwa wa kuvutia zaidi.

” Tumewekewa barabara za lami na TANROADS pamoja na mitaro mizuri sana iliyobaki ni kazi yetu kufanya mji wetu kuwa safi” alisema Luhanda Paul.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake