MLEZI wa CCM Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Naibu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza na Kamati za siasa ngazi za Kata,Wilaya ya Mpanda na Mkoa wa Katavi katika kikao cha ndani kilichofanyika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo.
BAADHI ya Wajumbe wa Kamati za siasa ngazi za Kata,Wilaya ya Mpanda na Mkoa wa Katavi wakisikiliza hotuba ya Mlezi wa CCM Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Naibu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa(hayupo pichani) katika mkutano wa ndani cha CCM kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda.
Na Is-haka Omar,Katavi.
Mlezi wa Mkoa wa Katavi na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema chama hicho kimejipanga kuhakikisha wagombea wake wa ngazi mbalimbali wanashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa nguvu ya kidemokrasia na ridhaa ya wananchi wa mkoa wa Katavi ndio itakayoiwezesha CCM kupata ushindi mkubwa.
Dkt. Dimwa aliyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za kata, mkoa, na wilaya pamoja na wagombea wateule na wale walioshindwa katika uchaguzi wa kura za maoni wa CCM, katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi. Ziara hiyo ilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Katika maelezo yake, Mlezi huyo wa CCM alieleza kuwa ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakuwa chimbuko muhimu cha kutathmini ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kwa ngazi za madiwani, wabunge, na Rais.
Alisisitiza kuwa CCM ina hakika ya kupata ushindi mkubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, ikiwemo uimarishaji wa sekta za afya, elimu, kilimo, uvuvi, na miundombinu ya barabara za kisasa, umeme, na huduma za mikopo kwa wajasiriamali wa makundi yote ya kijamii.
Katika mkutano huo, Dkt. Dimwa alikemea vikali makundi yanayoharibu umoja wa chama na kuwataka wanachama wa CCM kuwa wamoja.
Aliwataka wajumbe wa kamati za siasa kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya chama na kuhamasisha wananchi wote kuwapigia kura wagombea wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
"CCM ni chama kimoja, na hatuwezi kuwa na makundi yanayoharibu umoja wetu. Tunapaswa kuwa na mshikamano ili tuweze kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuleta maendeleo kwa wananchi. Msingi wa chama chetu ni umoja, na umoja ni nguvu," alisema Dkt. Dimwa.
Aidha, Dkt. Dimwa aliwahimiza wagombea wateule kutowadharau wagombea walioshindwa katika uchaguzi wa kura za maoni.
Alisisitiza kuwa kura za maoni ni sehemu ya mchakato na kwamba CCM ina nafasi kwa kila mmoja.
"Huu siyo mwisho wa safari yenu ya kisiasa, kura za maoni sio kipimo cha mwisho, bali ni sehemu ya mchakato. CCM ina nafasi kwa kila mmoja, wale walioshindwa wanapaswa kujivunia kwamba waligombea kwa heshima na kuendelea kuwa sehemu ya chama cha Mapinduzi," alisisitiza.
Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa viongozi wa CCM wanapaswa kuimarisha chama kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha wanatekeleza haki na usawa kwa wanachama wote. Aliwapongeza wazee, viongozi watendaji, na wanachama wa CCM wa Mkoa wa Katavi kwa juhudi zao za kuhakikisha chama na jumuiya zake zinaendelea kuimarika kila siku.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta, alieleza kuwa chama cha CCM kimejipanga kuhakikisha wagombea wote wanaopeperusha bendera ya CCM wanashinda kwa kishindo kutokana na mshikamano na umoja wa wanachama wa CCM katika mkoa huo.
Mwenyekiti wa Wilaya ya Mpanda, Joseph Lwamba, alisema licha ya changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa kura za maoni, wanachama, wagombea wateule, na wale walioshindwa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa.
Mbunge wa Jimbo la Mpanda, Sebastian Kapufi, alisema kuwa maandalizi ya kuhamasisha wanachama na wananchi kwa ujumla yanendelea vizuri ili kuikamilisha ushindi wa CCM.
Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Anna Lupembe, alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa katika mkoa wa Katavi na majimbo yake, ambapo wananchi wameendelea kujenga amani kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yao.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa, alieleza shukrani za wananchi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Shilingi Trioni 1.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo.
No comments:
Post a Comment