ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 28, 2024

TAARIFA YA MSEMAJI WA JESHI LA POLISI

JAMHURI MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI


JESHI LA POLISI TANZANIA                                                                             

TAARIFA KWA UMMA

Zipo taarifa kwenye Mitandao ya Kijamii na Vyombo vingine inayoonyesha kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, Roda Kunchela ikieleza kuwa, Mgombea wa Mtaa wa Miembeni Kilimahewa kupitia Chadema, Nsajigwa Mwandembwa alikamatwa na Polisi akiwa nyumbani kwake.

Aidha, ameeleza kuwa, huko katika eneo la Mwamkulu Ndg Herman Lutambi Mzee amepigwa hadi kivunjwa mkono na Diwani wa CCM.

Pia katika taarifa hiyo ameeleza kuna gari ndogo iliyotaka kumteka Ndg Christopher Kapaso aliyekuwa anagombea nafasi ya uenyekiti mtaa wa Kigamboni.

Jeshi la Polisi limefuatilia kwa kina ukweli wa taarifa hizo ili ikibainika ni za kweli hatua za kisheria zichukuliwe.

Baada ya ufuatiliaji huo sambamba na kuchukuwa maelezo ya watu mbalimbali, imebainika taarifa hizo ni za kutengeneza na  kuongeza chumvi ili kudanganya na  kupata huruma ya wananchi.

Ukweli uliopo kulingana na watu walioshuhudia ni kwamba Nsagigwa Mwandembwa mgombea kiti cha Mtaa wa  Miembeni Kilimahewa alikuwa akifanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura cha Miembeni na alionywa mara kadhaa lakini hakusikia. Baada ya kufikia hatua ambayo haivumiliki tena alikamatwa akiwa kwenye hicho kituo na kupelekwa kituo cha Polisi na kuhojiwa na bàada ya mahojiano na alipoona yeye mwenye athari ya vitendo vyake alidhaminiwa ili akakamilishe taratibu zake za uchaguzi kusubiri hatua zingine za kisheria.

Kuhusiana na taarifa aliyotoa kuwa, Ndg Herman  Lutambi Mzee amepigwa na Diwani wa CCM hadi kuvunjwa mkono ufuatiliaji wa kina umefanyika na imebainika kuwa, kilichokuwepo ni mzozo baina yao kulikosababisha kuchaniana shati na wala hajavunjwa mkono kama Mwenyekiti huyo anavyodanganya kwani mtu huyo leo amesafiri kutokà kijijini anakoishi na amewasili Mpanda Mjini mchana huu na kuelekea Ofisi ya Chadema Mkoa wa Katavi kwenye kikao na baada ya kikao hicho wakati wowote ule Mwenyekiti huyo wa Chadema ataongea na waandishi wa habari.

Kuhusu taarifa kuwa kulikuwa na jaribio la kumteka Ndg Christopher Kapaso, taarifa hizo zimefuatiliwa na hazina ukweli wowote.

Jeshi la Polisi, lingependa kutoa wito kwa baadhi ya Viongozi kama wana taarifa za kweli kufanyiwa uhalifu wowote wa kijinai waziwasilishe kupitia taratibu zilizopo za kisheria na kujiepusha kuandaa taarifa za uzushi na za uongo kwa nia ya kuihadaa na kuiaminisha jamii mambo ambayo hayapo kwani ni kiashiria tosha kuwa, lengo lao si kujenga bali ni kutaka kuvuruga amani, utulivu na usalama wa nchi yetu.


Imetolewa na:                                                              

David A. Misime - DCP

Msemaji wa Jeshi la Polisi

Makao Makuu ya Polisi

Dodoma,Tanzania                                                                            





www.polisi.go.tz      www.twitter.com/tanpol     www.facebook.com/PolisiTanzania      www.instagram.com/polisi.tanzania

No comments: