ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 29, 2024

TANZANIA KUNUFAIKA NA FEDHA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI


Kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa leo Novemba 29, 2024 jijini Dodoma akifungua Mkutano wa Kitaifa kuhusu mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29), uliofanyika Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Kanizio Manyika leo Novemba 29, 2024 jijini Dodoma akiwasilisha maazimio na matokeo ya mijadala ya mkutano na manufaa kwa Tanzania katika Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) uliofanyika Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan.

Washiriki wa Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) uliofanyika Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan, wakiwa katika mkutano wa mrejesho wa ushiriki wa mkutano huo, jijini Dodoma leo Novemba 29, 2024.
Washiriki wa Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) uliofanyika Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa mrejesho wa ushiriki, jijini Dodoma leo Novemba 29, 2029.

Tanzania imeahidiwa jumla ya Dola za Marekani milioni 782.2, Euro milioni 26, na Dola za Canada milioni 2 kutoka kwa washirika wa maendeleo duniani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ustahimilivu wa sekta mbalimbali.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 29, 2024 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja katika hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa kuhusu mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29), uliofanyika Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa amesema sanjari na hilo, pia mashirika na taasisi 30 zimeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, hususan katika biashara ya kaboni na juhudi za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Mkutano wa COP29 umekuwa wa kihistoria na fursa kwa Tanzania kwa kuzingatia matokeo na masuala yaliyofikiwa katika mkutano huo yakiwemo kuanza kufanya kazi rasmi kwa Mfuko wa Kushughulikia Hasara na Upotevu unaosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo imewezesha kufikiwa kwa lengo la kukusanya shilingi bilioni 300 kila mwaka hadi mwaka 2035 kutoka shilingi bilioni 100 kwa mwaka na kukamilishwa na kupitishwa kwa utaratibu wa biashara ya kaboni chini ya Kifungu cha 6 cha Mkataba wa Paris jambo ambalo linatoa fursa ya kipekee kwa Tanzania.
Aidha, Bi. Kemilembe amebainisha kuwa Tanzania iliingia katika mkutano huu ikiwa na ajenda na misimamo yake thabiti kuhusu Nishati Safi ya Kupikia na kusisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira kwa kupunguza utegemezi wa nishati zisizo salama za kupikia kama kuni na mkaa.
“Tulitoa wito wa kuongeza juhudi za pamoja ili kupunguza gesijoto duniani na kufanikisha lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani kuwa chini ya nyuzi joto 1.5 ifikapo mwaka 2030.
“Pia, Tanzania ilipata fursa ya kuonesha mafanikio ya utekelezaji wa hatua mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini. Juhudi hizi zinajumuisha miradi katika sekta za nishati, kilimo, uchumi wa buluu, na maji, pamoja na mipango mingine inayolenga kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi,” amefafanua Mkurugenzi Kemilembe.
Wakiachangia wakati wa mkutano huo, baadhi wa washiriki wa COP29 wameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu kwa ufanisi ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.

No comments: