Serikali imetoa shukrani za dhati kwa kundi la Mabalozi la nchi za Afrika nchini kufuatia uamuzi wa kundi hilo kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi milioni thelathini na nane kwa shule tatu za Sekondari ya Jangwani, Sekondari ya Pugu na Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu ambazo zina watoto wenye mahitaji maalum.
Shukrani hizo zimetolewa na Bi. Ellen Maduhu kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Desemba 03, 2024 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu ambayo husherehekewa kila Desemba 03.
Balozi Shelukindo alisema kuwa msaada huo wa Kundi la Mabalozi wa nchi za Afrika ni kitendo cha kupongezwa na ishara ya wazi ya kuonesha utu, huruma na mshikamano kwa watu wenye ulemavu. "Hiki kitendo kimeonesha maana kamili ya kuanzishwa kwa Siku ya Kuadhimisha Watu Wenye Ulemavu ambayo inalenga kutukumbusha jukumu letu la kibinadamu la kuwasaidia watu wenye ulemavu", Balozi Shelukindo alisema.
Balozi Shelukindo alieleza kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya ngazi ya kimataifa, kikanda na ya hapa nchini inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imekuwa ikitekeleza programu tofauti kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanaishi vizuri.
Balozi Shelukindo alimalizia hotuba yake kwa kuwahakikishia Mabalozi wa nchi za Afrika kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia uliopo na nchi zao kwa manufaa ya pande zote.
No comments:
Post a Comment