ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 4, 2024

SPIKA TULIA AWAKUMBUSHA WANADAMU KUTENDA MEMA.


Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ametoa wito kwa watanzania kufanya mema ili wakiondoka Duniani wazungumziwe vizuri.

Mheshimiwa Spika ametoa nasaha hizo wakati akitoa salamu za pole katika shughuli ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika Dkt. Faustine Ndugulile iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Kama alivyosema Baba Askofu kwamba sisi wote hapa duniani tupo safarini, lakini unafanya nini, tunayoyakusanya ni yepi ili siku kama ya leo watu wayaseme mema yetu, usikusanye mabaya,” alisema.

Mheshimiwa Spika alimshukuru Askofu aliyeendesha misa kwa mafundisho yake huku akisisitiza waombolezaji kukumbuka kufanya ibada ili watakapoondoka duniani viongozi wa dini waje kuendesha ibada kama walivyofanya kwa marehemu Dkt. Ndugulile.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowapa ushirikiano Watanzania wanaojitokeza na kuonyesha uwezo wao katika nafasi za kimataifa.

Alisema Mheshimiwa Rais amefanya hivyo kwake katika nafasi yake ya Rais wa IPU na kwa Mheshimiwa Dkt. Ndugulile.

“Napenda kuhukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kuweka bidii kuhakikisha Mheshimiwa Dkt. Nduguile anashinda nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, nafasi hii imeongeza heshimiwa kwa nchi yetu japo imekatizwa na kifo chake. Sina shaka utaendelea kufanya hivyo kwa watanzania wengine,”. alisema

Mheshimiwa Spika alitoa pole kwa Mheshimiwa Rasi, familia, ndugu na waombolezaji wote kwa msiba huo.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Meshimiwa Kassim Majaliwa mbali na kutoa pole alizungumzia jinsi alivyofanya kazi na marehemu kama Mbunge mwenzake na kama kiongozi wake serikalini.

“Nimemshuhudia alivyokuwa akiwapigania wananchi wake wa Kigamboni kwa moyo mmoja,” alisema.

Mheshimiwa Dkt. Ndugulile alifariki tarehe 27 Novemba, 2024 nchini India ambako alikuwa akipatiwa matibabu

No comments: