Paris, Ufaransa
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Saidi Othman Yakubu, amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Profesa Khaled El-Enany, katika Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Paris, Ufaransa.
Uwasilishaji huo wa hati unamwezesha Mhe. Balozi Yakubu kuanza rasmi majukumu yake kama Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya elimu, sayansi, utamaduni na mawasiliano.
Baada ya hafla hiyo, viongozi hao walifanya mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na UNESCO katika sekta za elimu, sayansi, utamaduni, uhifadhi wa urithi wa dunia pamoja na maendeleo ya rasilimali watu.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Yakubu aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kueleza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na UNESCO katika kutekeleza ajenda za maendeleo endelevu na kukuza ustawi wa wananchi kupitia elimu, sayansi na utamaduni.
Kwa upande wake, Profesa El-Enany amepongeza mafanikio na hatua za maendeleo zinazopatikana nchini Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kueleza kufurahishwa kwake na mchango wa Tanzania ndani ya UNESCO. Aidha, ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na UNESCO kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mkutano huo umeweka msingi mzuri wa kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na UNESCO katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.



No comments:
Post a Comment