ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 11, 2026

DKT. KIJAJI ASHIRIKI MKUTANO WA 126 WA BARAZA TENDAJI LA UTALII LA UMOJA WA MATAIFA HISPANIA



TOLEDO, Hispania 


JUNI 10, 2026


WAZIRI  wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameshiriki katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 126 wa Baraza Tendaji la Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa  (UN Tourism) uliofanyika katika mji wa Toledo, nchini Hispania.

Mkutano huo wa kimataifa umewakutanisha Mawaziri wa Utalii, Mabalozi na viongozi wa sekta hiyo kutoka nchi wanachama 35  kwa lengo la kujadili mwelekeo wa kimkakati wa shirika hilo katika kipindi kipya cha uongozi wa Katibu Mkuu mpya wa shirika hilo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Katibu Mkuu wa UN Tourism, Bi.  Shaikha Nasser Al Nowais, alitumia fursa hiyo kuelezea Dira ya Usimamizi ya shirika hilo itakayotumika kwa miaka minne kuanzia mwaka 2026–2029. Dira hiyo inalenga kuimarisha misingi ya taasisi, kuongeza uwazi na uwajibikaji na kuhakikisha shirika hilo linaleta matokeo chanya na yenye tija kwa nchi wanachama.

Kwa mujibu wa dira hiyo mpya, UN Tourism itaongozwa na kanuni tatu kuu: Kujenga misingi ya kudumu ya kitaasisi, Kuweka nchi wanachama katikati ya maamuzi na utekelezaji, na Kuhakikisha utoaji wa huduma unazingatia ubora na kina. 

Aidha vipaumbele vinne vilivyowekwa kwa kipindi cha 2026–2029 ni Misingi, Ushirikiano, Kuimarisha Ujuzi na Uendelevu.

“Hatua ya kwanza katika kipindi hiki kipya ni kuimarisha misingi ya shirika letu. Hakuna kipaumbele kinachoweza kutekelezwa kwa ufanisi bila kuwa na taasisi yenye uwazi, nidhamu ya kifedha na mifumo thabiti ya uwajibikaji,” alisema.

Vilevile, Bi. Al Nuwais alisisitiza kuwa Sekta ya Utalii ina mchango mkubwa katika uchumi wa dunia, ambapo inachangia takribani asilimia 10 ya Pato la Taifa la dunia na kutoa ajira kwa wananchi wa mataifa mbalimbali. 

Alibainisha kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanategemea uwepo wa taasisi imara, mifumo madhubuti ya usimamizi na ushirikiano wa karibu kati ya nchi wanachama.

Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo wa 126 wa Baraza Tendaji unaendelea kuimarisha nafasi ya nchi katika majukwaa ya kimataifa ya utalii na kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kukuza Sekta ya Utalii kama mhimili muhimu wa maendeleo endelevu.

Mkutano huo unafanyika kwa siku mbili na unatarajiwa kukamilika Jun 11,2026.











No comments: