Kwa mujibu wa simulizi la Frankata Thekiso, safari ya mwanamuziki Shabaan Yohana nchini Botswana ilianza miaka ya 1990, huenda kati ya 1996 au 1997, alipowasili huko kwa msaada wa Mtanzania mwenzake Nathaniel Mwamboma, maarufu kama Naya Capricorn.
Wakati huo Nata alikuwa akiongoza bendi ya Dar es Salaam Stars, iliyokuwa na makao yake katika ukumbi wa Sethegetsane, eneo la Mmopane, magharibi mwa jiji la Gaborone.
Katika kipindi hicho, Dar es Salaam Stars ilikuwa miongoni mwa bendi zilizokuwa zikifanya vizuri Botswana, huku ushindani wao mkubwa ukiwa bendi ya rumba iliyojulikana kama MOS & LED Sounds.
Shabaan Yohana alipojiunga na Dar es Salaam Stars, walirekodi santuri iliyoitwa Bula Maitho, iliyowafanya wajulikane zaidi katika medani ya muziki wa dansi nchini humo.
Hata hivyo, baada ya takribani mwaka mmoja, Dar es Salaam Stars ilisambaratika.
Shabaan hakukata tamaa. Badala yake, aliungana na wanamuziki wengine akiwemo Charlie, Evans Ngalube kutoka Zambia, na Mtanzania Ali Baba Kilunga kuanzisha kundi jipya lililoitwa Sakaye King. Kundi hilo lilikuwa likitumbuiza katika ukumbi maarufu wa Zebra Night Club, magharibi mwa Gaborone.
Ni katika kipindi hicho ndipo walipotoa santuri iliyotikisa sana yenye jina John O Nyala (yaani John Anaoa).
Wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa na kuvutia mashabiki wengi, huku nakala zake zikiuzwa kwa wingi.
Umaarufu wa Sakaye King uliendelea kukua, lakini baadaye Shabaan akaondoka na kujiunga na mwanamuziki mkongwe wa Botswana Frank Franco Lesokwane, pamoja na Mtanzania mwingine aliyejulikana kama Makambi.
Ushirikiano huo ulipelekea kuanzishwa kwa bendi ya Franco Afro Musica, ambayo ilikuja kuwa moja ya bendi maarufu zaidi Botswana.
Ndani ya bendi hiyo, Shabaan alikuwa mpiga gitaa la solo.
Umaarufu mkubwa ulipatikana kupitia kibao cha Ke Lela Le Lona, ambacho kilivuka mipaka ya Botswana na kusikika katika nchi jirani.
Baadaye walitoa nyimbo nyingine zilizopendwa kama Ba Ntolela Me Tshela na Robala Nana.
Mwaka 2004, Shabaan alihamia Selibe Phikwe na kujiunga na bendi ya Rainbow Sounds, ambako alitumikia kwa takribani miaka minne.
Hata hivyo, alirejea tena Afro Musica na kuendelea kuitumikia hadi mwaka 2008.
Wakati huo, mwaka 2005, Afro Musica ilimsajili mpiga solo mwingine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyejulikana kwa jina la Samurai Ngingo, ambaye alifanya kazi bega kwa bega na Shabaan.
Mbali na Afro Musica, mwaka 2006 Shabaan alifanya kazi pia na Extra Melody Band, bendi iliyokuwa imejitenga kutoka Afrika Sound na iliyokuwa na makao yake Mogoditshane.
Mwaka 2015 alipata changamoto ya kiafya, lakini baada ya kupona alirejea tena jukwaani na kujiunga na kundi la More Fire, ambalo lilitoa albamu ya Me Boela.
Katika miaka yake ya mwisho, aliendelea kuwa mwanamuziki wa More Fire huku akijihusisha pia na muziki wa injili.
Wale waliomfahamu wanamkumbuka Shabaan Yohana si tu kwa umahiri wake wa kupiga gitaa la solo, bali pia kwa utu wake wa kipekee.
@Alikuwa mtu mpole, mwenye heshima na aliyependwa na wengi ndani na nje ya tasnia ya muziki. Safari yake ya muziki nchini Botswana imeacha alama kubwa na inabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya wanamuziki wa Kitanzania waliovuka mipaka na kutamba katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.


No comments:
Post a Comment