Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikisha upasuaji wa saratani ya tezi dume kwa njia ya matundu madogo (Laparoscopic Radical Prostatectomy), teknolojia ya kisasa inayomwezesha mgonjwa kupata nafuu kwa haraka, kupunguza muda wa kulazwa hospitalini na kurejea kwenye shughuli zake za kawaida mapema.
Akizungumza baada ya kufanyika kwa upasuaji huo, Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo wa MNH, Dkt. Gift Daniel amesema mafanikio hayo yamepatikana kupitia kambi maalum ya siku mbili ya upasuaji na mafunzo kwa vitendo iliyowakutanisha wataalam wa mfumo wa mkojo kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma za kibingwa.
“Katika kambi hii tumefanyia wagonjwa 12 upasuaji wa changamoto mbalimbali za mfumo wa mkojo, ikiwemo saratani ya tezi dume, saratani ya figo, saratani ya kibofu cha mkojo, uvimbe wa maji kwenye figo (renal cyst) pamoja na huduma nyingine za kibingwa. Mafanikio haya yanaonesha uwezo wa wataalamu wetu kutumia teknolojia za kisasa katika kutoa huduma za ubingwa bobezi,” amesema Dkt. Gift.
Kambi hiyo imewakutanisha wataalamu kutoka Tanzania, China, Cameroon, DRC na Uganda, huku zaidi ya wataalamu wazawa 200 wakifuatilia upasuaji huo mubashara kwa njia ya mtandao, hatua iliyowezesha kubadilishana uzoefu na kueneza matumizi ya teknolojia za kisasa ya upasuaji wa mfumo wa mkojo katika hospitali mbalimbali vya afya.










No comments:
Post a Comment