Ukifika Makumbusho ya Taifa la Tanzania jitahidi sana kutana na Zinjanthropus boisei, mmoja wa Zamadamu wanaovutia zaidi ulimwenguni kote, anayejulikana kwa lishe yake maalum na maumbile ya kipekee sana kimwili hasa fuvu lake la kichwa na taya lake la mdomo wa chini na juu (upper and lower jaw).
Aliishi takriban miaka milioni 2.3 hadi 1.2 iliyopita katika eneo bonde la Olduvai Tanzania. Zinjanthropus boisei alistawi katika savanna na mazingira ya misitu ya wazi, akitegemea uwezo wake wa ajabu wa kutafuna chakula kigumu kama mbegu na mizizi ili kuishi.
Magego yake makubwa, na taya lake pana yaliunganishwa na misuli imara (masseter and temporalis muscles) iliyojishikiza kwenye fupa la upanga wa kichwa (suggital crest) ili kusaidia kutafuna chakula kigumu: vyenye nyuzi kama vile mizizi na mbegu ambazo *spishi zingine za Zamadamu* zingeweza kuepukwa. Ikumbukwe kwamba kuna nyakati Mheshimiwa Zinjanthropus boisei aliishi sambamba na Homo habilis wakiwa pamoja katika mazingira hayo ya Olduvai.
Tofauti na mwenzake Homo habilis, Zinjanthropus boisei huenda hakutegemea sana zana za mawe, badala yake alitegemea viungo vyake vya kimwili ili kuchakata chakula kwa ufanisi hasa mikono na mdomo. ZINJ huyu mwenye nguvu thabiti leo amepumzika zake yuko hapa *Makumbusho ya Taifa Dar-es-Salam*, anatunzwa vema na amehifadhiwa kisasa kabisa. Ukimtizama ndani ya *kasha lake la dhahabu* akiwa amevaa *medali yake aliyotunukiwa*, anaonesha utofauti wake yeye na Zamadamu wengine wa awali na mageuzi ya njia nyingi alizozichagua yeye katika jitihada za kuendelea kuishi.
Kila kukicha mifupa yake husimulia hadithi ya ustahimilivu na utaalam, inayoonyesha jinsi Zamadamu wa mwanzo walizoea mazingira yao muda mrefu kabla ya ugunduzi moto, uwindaji, au zana za mawe na chuma kuanza kuenea.
🌍 Kutoka Makumbusho ya Taifa la Tanzania Muheshimiwa Paranthropus boisei anatukumbusha kwamba mageuzi ya binadamu (human Evolution) si mstari ulionyooka bali ni hadithi ya majaribio mengi, yaliyozaa matawi ya kuishi kwao Kutoka shina moja la mageuzi hadi matawi tofauti. Yapo matawi yaliyotoweka na mengine yalifanikiwa kuwa endelevu. Moja ya tawi lililotoweka ni hili la Babu Zinj.
Kwa kifupi mifupa ya Zinjanthropus boisei inaongea maneno mengi, siwezi simulia yote nikamaliza. Nawakaribisha sana mtembelee Makubusho ya Taifa la Tanzania muonane naye *Zinj* mwenyewe, msikilize wenyewe kwakuwa *mifupa yake huwa inaongea*.

No comments:
Post a Comment