Kilele cha Tamasha la Bulabo Kanda ya Ziwa 2026 kilichofanyika katika Viwanja vya Ngomeni, Kisesa – Mwanza, kimeacha funzo kubwa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi utamaduni, kuimarisha umoja na kujenga maridhiano kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki kwa mafanikio makubwa ni Taasisi ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA ORGANIZATION), ambayo imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuunganisha Watanzania kupitia misingi ya uzalendo, mshikamano na amani.
Mgeni rasmi wa tamasha hilo, Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliyemwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chifu Hangaya, aliwapongeza machifu wa jadi kwa kuendelea kuhifadhi na kurithisha mila, desturi na maadili mema ya Kitanzania.
Alisisitiza kuwa utamaduni wetu unatufundisha kuheshimiana, kusikilizana na kutafuta suluhu za tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo. Huo ndio msingi wa kudumisha amani, mshikamano na maendeleo endelevu katika Taifa letu.
Kaulimbiu ya Tamasha la Bulabo 2026 iliyosema:-
"MARIDHIANO KWA NJIA YA AMANI NDIYO JADI YETU, LINDA MAADILI YA MTANZANIA"
imebeba ujumbe mzito unaohitaji kuendelea kuishi mioyoni mwa Watanzania wote. Leo zaidi kuliko wakati mwingine wowote, Taifa linahitaji watu wanaojenga madaraja ya upendo badala ya kuta za migawanyiko; watu wanaotanguliza maridhiano badala ya migogoro; na watu wanaolinda maadili ya Kitanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ushiriki wa PATUTA ORGANIZATION katika tamasha hili ni ishara kwamba taasisi na wananchi wana nafasi kubwa ya kuendeleza utamaduni wa amani, umoja na uzalendo. Kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza, wanachama wa PATUTA waliungana kuonesha kuwa nguvu ya Taifa lolote ipo katika mshikamano wa watu wake.
Tamasha la Bulabo 2026 limetukumbusha jambo moja muhimu: Tofauti za mawazo si sababu ya chuki, bali ni fursa ya kujenga maelewano. Tukidumisha amani, tukalinda maadili yetu na kuendeleza utamaduni wa kusikilizana, Tanzania itaendelea kuwa mfano wa umoja na utulivu barani Afrika.
Hongereni PATUTA ORGANIZATION kwa kuwa sehemu ya ujumbe huu mkubwa wa kitaifa.
PAMOJA TUTASHINDA TANZANIA
"Umoja hutujenga, amani hutudumisha, na maridhiano hutuvusha kwenda kwenye maendeleo ya kweli."
Imetolewa na:-
Cde JAMAL ALLY
Katibu Mkuu PATUTA ORGANIZATION




No comments:
Post a Comment