Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, amewataka wafamasia wa hospitali hiyo kuendana na kasi ya mabadiliko yanayoendelea kufanyika katika taasisi hiyo na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuelekea Muhimbili mpya yenye huduma bora na za kisasa kwa wananchi.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Wafamasia yanayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Juni 10 hadi 16, Dkt. Kimambo alisema ni muhimu kwa wataalamu hao kuelewa mwelekeo wa maboresho yanayotekelezwa hospitalini, kutambua mahitaji ya Muhimbili mpya na kutoa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kufanikisha mabadiliko hayo. Alisisitiza kuwa mafanikio ya mageuzi hayo yanategemea ushirikiano, ubunifu na utayari wa watumishi kuyapokea na kuyasimamia kwa pamoja.
Aidha, Dkt. Kimambo alihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya wafamasia na kada nyingine za afya ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu salama na yenye ubora unaokusudiwa.
Kwa upande wao, wafamasia wameishukuru Serikali pamoja na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya famasi kupitia uwekezaji unaofanyika katika upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na miundombinu ya kisasa inayorahisisha utoaji wa huduma. Wamesema hatua hizo zimekuwa chachu ya kuimarika kwa huduma na kuongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Maadhimisho ya Wiki ya Wafamasia mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, Famasi: Ufunguo wa Maono ya 2050 katika Sekta ya Afya, ikisisitiza nafasi muhimu ya taaluma ya famasi katika kufanikisha maendeleo ya huduma za afya nchini.





No comments:
Post a Comment