Tuzo za Malkia wa Arusha 2026 zimewakutanisha wanawake zaidi ya 300 kutoka sekta mbalimbali nchini kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wao katika maendeleo ya jamii na uchumi. Katika hafla hiyo, wanawake 30 vinara walitunukiwa tuzo kwa umahiri wao katika sekta mbalimbali ikiwemo Ujasiriamali, Biashara, Kilimo, Utalii, Afya, Elimu, Teknolojia, Maendeleo ya jamii, Sanaa na Utamaduni. Hafla hiyo ilifanyika tarehe 27 Juni 2026 katika Hoteli ya Gran MeliĆ” Arusha.
Akimwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Mgeni Rasmi ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Witness Shoo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha, aliwapongeza wanawake wote walioshiriki na waliotambuliwa kwa mchango wao katika jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi alisema ongezeko la watalii nchini linafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa watanzania hususan wanawake na kuwataka kujipanga kunufaika na matukio makubwa yanayotarajiwa kufanyika nchini, ikiwemo Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union - IPU)2026, World Travel Awards Grand Finale 2026 na AFCON 2027, kwa kujiandaa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa ili kuongeza mapato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Vilevile, aliwahimiza wanawake kuendelea kudumisha nidhamu, uadilifu, ushirikiano na kujituma, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo ya kujenga viongozi bora, jamii yenye maadili na uchumi imara.
Kupitia jukwaa hilo, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) liliendelea kuhamasisha Utalii wa ndani pamoja na kutangaza fursa mbalimbali za Utalii na uwekezaji zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa Tanzania.
#MalkiaWaArusha #TuzoZaWanawake #TanzaniaParks #ATM2030 #UtaliiNiMaisha #DestinationTanzania















No comments:
Post a Comment