ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 28, 2026

WAHADZABE KWA MARA YA KWANZA KATIKA HISTORIA JUKWAA LA ZIFF2026


Uchezaji na burudani ya kipekee kutoka kwa jamii ya asili ya Wahadzabe ilikuwa moja ya vionjo vilivyoteka hisia za watazamaji zaidi ya 300 katika ufunguzi wa msimu wa 29 wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF 2026).

Onyesho lao lilianza kwa namna ya kipekee ambapo, kabla ya kuingia kwenye ngoma yenyewe, waligubika jukwaa kwa mchezo wa kuigiza ulioonesha uhalisia wa maisha yao ya kila siku ya nyumbani na uwindaji. 

Taswira hiyo ya asili ilivutia mno na kuwafanya watazamaji kubaki vinywa wazi kwa mshangao na msisimko mkubwa.  

Baada ya kuonesha tamaduni hizo za maisha ya kila siku, burudani hiyo iligeuka kuwa sherehe kubwa pale walipoanza kushangilia maisha yao kupitia ngoma ya jadi yenye miondoko ambayo ni nadra sana kuikuta nje ya mazingira yao ya asili. 





Ilikuwa ni midundo ya kusisimua iliyosababisha jukwaa zima kutikisika kwa nguvu ya miguu yao na hewa kujazwa na mikono iliyokuwa ikitinga kwa madaha. 

Shangwe hiyo ilipamba moto kiasi cha kumfanya Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola, pamoja na viongozi wakuu wa ZIFF, kushindwa kuzuia hisia zao na kujumuika nao jukwaani kucheza na kushangilia pamoja midundo hiyo adhimu ya kitamaduni.  

Tamasha la ZIFF2026 mwaka huu linafanyika Juni 24-28, 2026.

Kwa hisani ya BSKY media, Zanzibar.










No comments: