ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 9, 2026

ASYA IDAROUS KHAMSIN AWAOMBA DIASPORA KUWASHIKA MKONO YATIMA: VID YACHANGISHA MILIONI 40 KWA VIFAA VYA SHULE NA FUTARI 2027

 


Mama Mlezi wa VID Bi. Asya Idarous Khamsin akiwa na mshehereshaji kunadi vitu mbalimbali katika harambee ya kuchangia Fedha kwa wahitaji hususani Yatima 


Dar es Salaam:


Taasisi ya Wanawake wanaojitolea kwenye maendeleo ya 'Volunteers In Development' (VID) chini ya Mama Mlezi wake Mama wa mitindo Bi. Asya Idarous Khamsin imepata Shilingi Milioni 40 kwenye Harambee ya kuchangisha vifaa vya shule kwa mwaka mpya wa masomo (Back to school) na mahitaji ya futari kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani 2027 kwa familia zinazolea yatima wa majumbani na wenye uhitaji.

Tukio hilo limefanyika November 8, 2026 katika ukumbi wa Golden Jubilee Tower, Jijini Dar es Salaam ambapo bidhaa ziliweza kunadiwa na watu kuweza kununua kuchangia mahitaji hayo.

Awali, Mama Mlezi wa VID, Asya Idarous Khamsin amewashukuru wadau kwa kuendelea kuwashika mkono huku pia akiendelea kuwaomba Watanzania na Diaspora waliopo nje ya Tanzania kuendelea kuwashika mkono katika kugusa Yatima.

Kwa upande wake Rais na Mwenyekiti wa VID, Bi. Tune Salim amewashukuru wahisani na wadau wote waliojumuika kwa pamoja katika zoezi hilo la harambee kwani linaenda kuwagusa wenye uhitaji.

"Ukiwa kama mhisani wetu unayependa kumkopesha Mwenyezi Mungu, tunashukuru kwa mchango wako wa hali na mali ikiwemo walionunua bidhaa hizi kwenye harambee kufanikisha jambo hili, ili familia zinazolea yatima na wenye uhitaji zipate matumaini ya furaha ya mwaka mpya wa masomo na kuweza kufunga Mwezi Mtukufu kwa utulivu na furaha." Amesema.

Nae Meneja wa VID, Bi. Haitham Ahmed Daudi katika kupunguza machungu ya ukali wa maisha kwa watoto yatima, amesema lengo ni kukusanya fedha zaidi ya Milioni 145.

"Fedha zinaenda kusaidia programu za shule na shughuli za mwezi wa Ramadhani, kwa kuhudumia Yatima Zanzibar na Tanzania Bara ambapo watoto Yatima 953 na tuna familia 680 zinazohitaji sadaka yako mwezi mtukufu wa Ramadhani." Amesema.

Aidha, amesema mbali na harambee hiyo, bado milango ipo wazi ambapo watu mbalimbali, taasisi na kampuni na washirika wa ndani na nje wanaweza kuchangia vitu kama vyakula, vifaa na Fedha taslimu.

"Elimu kila Mtoto mmoja ni Tsh 85,000 na kwa ramadhani kila familia ni Tsh 90,000. Tunapokea vifaa, tunapokea vyakula na tunapokea fedha kiasi chochote.

Lakini unaweza kutupigia ama kuchangia kupitia:

Yas Mixx: +255 655 900 444, Airtel Money: +255 789 407 887,

Mpesa: +255 768 587 488

Au M-PESA LIPA NAMBA: 52994606

Jina: VOLUNTEERS IN DEVELOPMENT,

Yas Mixx LIPA NAMBA: 22162201

Jina: VOLUNTEERS IN DEVELOPMENT". Amebainisha.

VID imeanzishwa mnamo mwaka 2012 ikijihusisha zaidi kwenye elimu ya watoto Yatima waishio na familia zao (Babu, Bibi, Mjomba, Shangazi n.k) imekuwa ikiandaa matukio mbalimbali ya kuchangisha Fedha kwa wahitaji hususani Yatima.

Tukio hilo limewezeshwa na wadhamini mbalimbali: New Rothmana Caterers, Milele Bookhouse, Hightham Technologies, Amazing Food, Ladeedah, Yakubu & Associates Chamber, Belcol Partners, Ladeedah Lux, Fabak Fashions - Asyakhamsin, MYOD - Make Your Own Destiny, Noor Al Mustafa, Makh's Bistro, MOE - Master One Energies Limited na wengine wengi.





































Friday, November 6, 2026

SERENGETI KUWA MWENYEJI WA TUZO ZA DUNIA ZA UTALII (WORLD TRAVEL AWARDS)



London, Uingereza, Novemba 5, 2026


Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika ramani ya utalii duniani baada ya kutangazwa kuwa mwenyeji wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards – WTA) kwa mwaka 2026, zitakazofanyika Desemba 12, 2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Tangazo hilo limetolewa Novemba 5, 2026 na Mwanzilishi na Rais wa World Travel Awards, Bw. Graham Cooke, wakati wa hafla maalumu iliyofanyika katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya World Travel Market (WTM) jijini London, Uingereza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Cooke amesema Tanzania imechaguliwa kutokana na upekee wake katika sekta ya utalii, akibainisha kuwa Serengeti ni moja ya majina makubwa yanayotambulika barani Afrika na duniani kutokana na utajiri wake wa wanyamapori na vivutio vya kipekee.

Ameongeza kuwa uwepo wa Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika, pamoja na uzuri wa vivutio vya asili na ukarimu wa Watanzania, ni miongoni mwa sababu zilizoifanya Tanzania kuwa chaguo sahihi la kuandaa tukio hilo la kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amemshukuru Bw. Cooke na taasisi ya World Travel Awards kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa hafla hiyo muhimu, akieleza kuwa nchi ipo tayari kuhakikisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wanapata uzoefu wa kipekee wa utalii wa Tanzania.

Amesema Serengeti nayo ipo tayari kupokea wageni zaidi ya 500 wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani, huku akisisitiza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania, kuongeza muonekano

wake kimataifa na kuimarisha nafasi yake katika soko la utalii duniani.

Aidha, Dkt. Kijaji ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi na uongozi wake katika kuifungua Tanzania na kuimarisha diplomasia, akisema kazi kubwa inayofanyika chini ya uongozi wake imechangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi katika jukwaa la kimataifa la utalii.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Dkt. Thereza Mugobi.







Tuesday, November 3, 2026

DKT. KIJAJI AONGOZA MAZUNGUMZO YA KUKUZA UTALII WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA

 

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, ametua jijini London, Uingereza, kwa ajili ya kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya WTM London 2026 yanayotarajiwa kufanyika Novemba 3–5, 2026.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, akiwa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Kijaji leo Novemba 2, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa utalii kwa lengo la kujadili fursa na mikakati ya kukuza na kuitangaza Tanzania kama kituo cha utalii katika soko la kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kijaji amepokea wasilisho kuhusu utalii kutoka kwa Bw. Tim Henshall, Afisa anayeshughulikia masuala ya Utalii katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza (Tanzania High Commission UK).

Aidha, amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Craig Rix, Mtendaji Mkuu wa Gecko Publishing, ambapo wamejadili fursa za kuitangaza Tanzania kupitia machapisho ya Gecko Publishing, ikiwemo jarida la Travel Africa Magazine, ili kuongeza mwonekano wa vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Katika kikao kingine, Dkt. Kijaji amekutana na Bw. George Bartlam, Meneja wa Mauzo ya Ubia wa Klabu ya Soka ya Brentford (Brentford Football Club) ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 6 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo wamejadili uwezekano wa kutumia klabu hiyo kuitangaza Tanzania.

Vikao hivyo vimehudhuriwa pia na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Bw. Patrick Mwakalobo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi. 

Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii za kupanua wigo wa ushirikiano na wadau wa kimataifa, kubuni njia bunifu za kuitangaza Tanzania na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.