Rais wa Chile, Michelle Bachelet, amesema watu wapatao millioni mbili wameathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea nchini humo siku ya Jumamosi.Zaidi ya watu mia tatu wamethibitishwa kufariki dunia katika janga hilo.
Tetemeko hilo lenye kiwango cha 8.8 katika vipimo vya majanga hayo, lilisababisha mawimbi ya tsunami katika eneo nzima la Pacific, ingawa mawimbi hayakuwa makubwa kama ilivyotabiriwa hapo awali.
Ni tetemeko kubwa zaidi kutokea Chile katika kipindi cha miaka hamsini.
Uharibifu mkubwa wa barabara na majengo umeripotiwa katika maeneo mengi, ukiwemo mji mkuu, Santiago, ambako kiwanda cha kemikali kilishika moto.
Hakuna huduma muhimu kama vile mawasiliano ya simu, maji na umeme.
Picha za televisheni zilionyesha daraja kubwa mjini Concepcion ambalo lilianguka katika mto wa Biobio, huku makundi ya waokoaji yakiendelea kuwatafuta manusura katika majengo yaliyoanguka.
Wafungwa zaidi ya mia mbili nawo waliweza kutoroka jela katika mji wa Chillan, lakini 60 kati yao walikamatwa tena na vikosi vya usalama.
Rais Barack Obama alisema Marekani iko tayari kutoa msaada iwapo serikali ya Chile itatoa ombi rasmi.
No comments:
Post a Comment