IDADI ya watu waliokufa kwenye ajali ya basi la AM Coach iliyotokea juzi wilayani Nzega, imefikia 26, baada ya wengine wawili kufariki dunia jana, huku maiti 18 wakitambuliwa na ndugu zao.
Kutokana na kutambuliwa kwa miili hiyo, hadi kufikia jana mchana, maiti wanane walikuwa hawajatambuliwa na wanaendelea kuhifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Nzega, kutokana na marehemu hao kutokuwa na vitambulisho vyovyote.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, maiti hao 18 walitambuliwa kwa vitambulisho vya kazi, vya kura na kadi za benki.
Kamanda Barlow aliwataja waliotambuliwa hadi jana kuwa ni Faustine Simon wa Katesh, Manyara; Pastory Kaiza; Epelanya Mleke; Gerald Nyitwe ambaye ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Kikosi cha 39 Arusha; Julieth Rupia wa Mwanza na Stephen Malolo wa Shinyanga.
Wengine ni Noel Munisi; Paul Boniface wote wa Manyara; Ritha Thomas wa Moshi; Magreth Asenga (Moshi); Elizabeth Uriki ambaye ni Mtawa wa Kanisa Katoliki (Mwanza); Salome Richard (Babati); Doria Agai (Mwanza); Joachim Paul (Nzega); James Agai (Mwanza); Abeid Ngayanimo (Nzega), Milambo Benjamin (Nzega) na Benson Ochieng.
Aidha, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk. John Mombeki, alisema majeruhi wanne waliovunjika miguu na mikono walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa tiba zaidi baada ya madaktari wa hospitali hiyo kukosa uwezo wa kutoa matibabu zaidi kwa majeruhi hao.
Aliwataja majeruhi waliokimbizwa Bugando kuwa ni Nakijiwa Ibinga wa Same Kilimanjaro; Prosper Magacha (Hanang); Joyce Nyanda (Nyakato - Mwanza) na Chega Msila (Mwanza). Dk Mombeki alisema majeruhi wengine wawili waliokuwa wakikimbizwa pamoja nao kwenda Bugando, walifariki dunia njiani, hivyo kufanya idadi yao kuwa 26 baada ya juzi watu 24 kufa papo hapo katika ajali hiyo iliyotokea kati ya Kitangiri na Migua kiasi cha kilometa 12 kutoka Nzega mjini.
Alisema kulingana na taarifa za kitabibu, majeruhi wengine sita wanatarajiwa kusafirishwa kwenda Bugando kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment