ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 1, 2010

Wapinzani:"Museveni amuandaa mwanawe"

Rais Museveni na mwanawe Luteni Kanali Kainerugaba Muhoozi
Chama kikuu cha upinzani nchini Uganda kimemshutumu Rais Yoweri Museveni kwa kumuandaa mwanawe achukue nafasi yake mara atakapoachia madaraka.
Mwanawe Museveni Luteni Kanali Kainerugaba Muhoosi ambaye tayari alikuwa mkuu wa kikosi maalum cha jeshi, sasa amepewa wadhifa mwengine wa kuongoza kikosi cha walinzi wa Rais.
Kwa mujibu wa msemaji wa upinzani Hussein Kyanjo, Rais Museveni anaifanya nafasi ya Urais Uganda iwe ya kurithiana baada ya wao kuona wazi anamuandaa mwanawe.
Watu kadha wa ukoo wa Museveni wanashikilia nafasi za juu serikalini.
Hata hivyo msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulaigye amekanusha tuhuma hizo baada ya kuteuliwa Muhoozi.
Amesema Muhoozi hajafanya kosa lolote la jinai kwa kuwa mtoto wa Rais. Yeye ni mtu kama Waganda wengine akiwa na haki zote ikiwemo ya kugombea Urais iwapo atapenda.
Luteni Kanali Muhoozi mwenye umri wa miaka 36 aliteuliwa kuongoza kikosi maalum mwaka 2008. Amepata mafunzo ya kijeshi Uingereza na Marekani.

No comments: