Hatma ya kisiasa nchini Sudan, haijulikani, kufuatia kujiondoa kwa mwakilishi wa chama kikuu cha upinzani katika uchaguzi mkuu wa urais utakaofanyika April 11.Yassir Arman alikuwa anawakilisha chama cha SPLM, waliokuwa waasi kusini mwa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi baada ya miaka 25.
Rais Omar Al Bashir ametishia kufutilia mbali kura ya maoni kuhusu kujitawala kwa Sudan Kusini, ikiwa chama hicho cha SPLM kitajiondoa kutoka kwa uchaguzi huo.
Viongozi wa chama hicho wamesema wamejiondoa kwa sababu hawaamini kuwa uchaguzi wa urais utakuwa huru na wa haki.
Hata hivyo chama cha SPLM kitashiriki katika uchaguzi wa ubunge na baraza ya miji katika maeneo yote isipokuwa lile la Darfur, ambako mapigano yanaendelea.
Kiongozi wa chama cha SPLM Salva Kirr ambaye ni Makamu wa Rais wa Sudan, ameiambia BBC kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya uchaguzi huo mkuu na kura ya maoni kuhusu kujitawala kwa Sudan Kusini.
No comments:
Post a Comment