na Betty Kangonga
KAMATI ya Umoja wa Vijana ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), imemtaka Mufti wa Tanzania Sheikh Mkuu, Issa bin Shaban Simba, kuwaondoa katika nafasi viongozi wawili wa umoja huo kutokana na ubadhirifu wa fedha za umoja huo.Viongozi hao ambao wanadaiwa kushiriki ubadhirifu huo ni Mweka Hazina, Ali Mbwera, na Mjumbe wa Kamati hiyo, Hassan Juma, kwa vile wamesababisha kamati nzima kuonekana imeshindwa kuwajibika ipasavyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, msemaji wa kamati hiyo, Ramadhani Iddi, alisema viongozi hao wanatakiwa kuondolewa kutokana na kushindwa kuenda na kasi ya utendaji kazi.
Alisema Mweka Hazina anatakiwa kuchukuliwa hatua zinazostahili ili kukomesha tabia za matumizi mabaya ya fedha za ofisi hizo.
“Tulikabidhiwa kiasi cha sh milioni moja na BAKWATA kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi wa kamati ya vijana lakini mweka hazina aliondoka na laki tano bila kuupa taarifa uongozi juu ya matumizi ya fedha hizo,” alisema Iddi.
Alisema kamati hiyo, iliteuliwa mwanzoni mwa mwaka huu na Mufti Simba na ilitakiwa kuzinduliwa Aprili 5 mwaka huu lakini mambo yameendelea kuwa magumu.
“Ingawa tunakabiliwa na mambo mengi, huku yakiwepo matatizo yaliyojitokeza, tulichanga fedha na kuzindua kamati kwa fedha zetu, lakini kitendo cha kutumia fedha za uzinduzi ni kinyume na maadili, hivyo inatakiwa Mufti awachukulie hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kuwatimua katika nafasi hizo,” alisema Idd.
No comments:
Post a Comment