
SIKU moja baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM, kugombea urais wa Zanzibar na kulalamikia hoja ya kubaguliwa kwa misingi ya rangi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, amefichua siri kwamba hakunyonya ziwa la mama yake mzazi bali la mama Mzanzibari (Mwafrika) baada ya kuzaliwa.
Amesema si yeye pekee, kaka yake Mustapha na mdogo wake Yunus, pia walinyonya maziwa ya mama Wazanzibari baada ya kuzaliwa.
Alisema hatua hiyo inatokana na mama yao mzazi, Rehemat Abdulhaman kuwa na matatizo ya kushindwa kutoa maziwa kila alipojifungua.
Haroun alilazimika kufichua siri hiyo ambayo anasema hajawahi kuisema tangu udogo wake, baada ya kuwapo hoja kwamba ni Mhindi na hivyo hawezi kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Zanzibar.
Alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu katika Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui mjini hapa Jumatatu iliyopita, pamoja na mambo mengine, Haroun alisikitikia hoja hiyo aliyodai kuwa inajengwa na wapinzani wake kisiasa, ambao wameshindwa kuona kasoro nyingine kutokana na sifa na utendaji wake.
“Watu wanasema mimi Mhindi. Sawa, ngozi yangu ndivyo ilivyo, sikuomba kwa Mungu kuzaliwa na ngozi hii. Najua tatizo ni azma yangu ya kugombea urais, ndiyo inayosababisha leo nibaguliwe.
“Nimekuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa miaka 10 sikusikia hili, nimekuwa Waziri kwa miaka 10 sikulisikia hili na nimekuwa Mbunge kwa miaka mitano sikulisikia hili,” alisema Haroun.
Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri Haroun alifanya mahojiano maalumu na HABARILEO na kutoboa siri kuwa aliwahi kunyonya maziwa ya mama mweusi na ndiyo maana tabia na mwenendo wake vinatofautiana na Wahindi wengine.
“Mama yangu (Rehemat) ana matatizo ya kutotoa maziwa anapojifungua, mimi nilipozaliwa mama hakuwa na jinsi, alimwomba jirani yake anayeitwa Mariam aninyonyeshe, ili kuokoa maisha yangu na aliendelea kuninyonyesha kwa wiki kadhaa, hadi mama alipoanza kutoa maziwa na mimi kuanza kunyonya maziwa yake.
“Kaka yangu Mustapha yeye alinyonya ziwa la mama mmoja anaitwa Mwanajasi na mdogo wangu Yunus alinyonya ziwa la Fatma mke wa marehemu Ally Vuai,” alisema Haroun aliyezaliwa Julai 24, 1953, Makunduchi, Zanzibar.
Alipozungumza na waandishi wa habari, Waziri Haroun alisema yeye ni Mzanzibari anayekubalika na Wazanzibari wengi na hakukurupuka alipojitokeza kutangaza nia na hatimaye kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Zanzibar.
Alisema anajiamini kuweza kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio kutokana na uzoefu aliosema ameupata kutoka kwa Rais Amani Abeid Karume na Rais Jakaya Kikwete ambao alisema ameshirikiana nao bega kwa bega katika uongozi wake.
Katika hatua nyingine Haroun alisisitiza, kwamba kama hatapata nafasi hiyo ya kuwania urais wa Zanzibar, atarudi kijijini kwake Makunduchi kuomba ridhaa ya kuendelea kuwatumikia katika nafasi ya uwakilishi na atamuunga mkono kwa dhati atakayeteuliwa.
No comments:
Post a Comment