
KIUNGO mahiri wa zamani wa Nigeria, Austin ‘Jay Jay’ Okocha
Na Saleh Ally, JohannesburgKIUNGO mahiri wa zamani wa Nigeria, Austin ‘Jay Jay’ Okocha amesema pamoja na kwamba soka ni mchezo unaohusiana na makosa, lakini kiungo wa timu hiyo San Kaita anapaswa kulaumiwa kutokana na timu yake kupoteza mchezo dhidi ya Ugiriki.
Pamoja na Nigeria kutangulia kupata bao, ililala kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya Kaita kutolewa nje katika dakika ya 32 kutokana na kumkayanga na kumsukuma makusudi beki wa Ugiriki huku mpira ukiwa nje ya mchezo.
Akizungumza mara baada ya mechi hiyo mbele ya waandishi mbalimbali wa afrika walioalikwa kwenye ofisi za Shirika la Habari la Afrika Kusini (SABC) jijini hapa, Okocha alisema alichoonyesha Kaita ni kitu kinachopaswa kulaumiwa, lakini akaomba apewe nafasi kujirekebisha.
“Ni kitu kinachoumiza sana, unaweza kuona mambo kama ni ya kawaida lakini mimi hadi nashindwa kuzungumza. Roho inaniuma na sielewi Keita alikuwa anafikiria nini kufanya hivyo, ni kitu kigumu kwa kweli.
“Anapaswa kulaumiwa, lakini apewe nafasi ya kuona kiwango cha upuuzi alichokifanya kiliathiri kiasi gani taifa lake na baada ya hapo, pia apewe nafasi ya kujirekebisha. Wako wengi ambao wamewahi kufanya hivyo lakini baadaye walijirekebisha na mambo yakaenda vizuri tu,” alisema Okocha.
“Nafasi ya Nigeria kwa kawaida inaweza kuwa finyu, lakini kimpira na kundi walilopo inawezekana wakawa na nafasi ya kusonga hatua ya 16 bora, lakini wanatakiwa kushinda kwa mabao mengi.
“Sijui nini kitatokea mbele, lakini yote hayo ni sehemu ya mambo ambayo hutokea kwenye soka, hayazuiliki,” alisema Okocha ambaye yuko nchini hapa kwa mwaliko wa SABC pamoja na nyota wengine mbalimbali.
Nigeria iko katika kundi B na timu za Ugiriki, Korea Kusini na Argentina na inatakiwa kushinda mechi ya mwisho kwa zaidi ya mabao mawili huku ikisubiri Argentina iibabue Ugiriki ili iweze kusonga mbele. Mechi yake ya kwanza ililala kwa bao 1-0 dhidi ya kikosi cha Diego Maradona, Argentina.

No comments:
Post a Comment