
Kocha mpya wa Taifa Stars, Jon Poulsen
Na Mwandishi Wetu UJIO wa Kocha mpya wa Taifa Stars, Jon Poulsen umekuwa pigo kubwa kwa timu kubwa za Simba na Yanga baada ya kutoa mapendekezo ambayo yanaziweka klabu hizo kwenye wakati mgumu.
Kocha huyo anakuja kuchukua nafasi ya Mbrazili, Marcio Maximo ambaye amemaliza kipindi chake cha miaka minne cha kuitumikia Taifa Stars, na anatarajiwa kuanzia kazi rasmi mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kocha huyo ametoa mapendekezo kadhaa ambayo ni pigo kubwa kwa Simba na Yanga.
Moja ya mambo aliyopendekeza Poulsen, ni kanuni mpya ambayo TFF wameshaitangaza kuwa itatumika kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kuwa klabu zote za ligi hiyo zinatakiwa kusajili wachezaji wa nje wasiozidi watano, kanuni ambayo ilipingwa vikali na makocha wa timu zote mbili, Patrick Phiri wa Simba pamoja na Kosta Papic wa Yanga.
Lakini pia taarifa zinasema kocha huyo amependekeza kanuni nyingine ndani ya shirikisho hilo, akitaka timu zisajili wachezaji watano wenye umri chini ya miaka 20, na iwe inawatumia wawili kwenye kila mchezo. Kanuni hiyo imeelezwa kuwa, itaanza kutumika mara baada ya msimu ujao wa ligi .
“Kanuni hii haitatumika msimu ujao, lakini baada ya kumalizika kwa ligi itatangazwa kwa ajili ya ligi ya msimu wa 2011/2012 nia ni kuhakikisha tunakuwa na timu nzuri ya taifa na haya ni mapendekezo ya kocha mpya,” kilisema chanzo hicho.
Poulsen ambaye ni raia wa Denmark, ni kocha mwenye uwezo wa hali ya juu wa kufundisha vijana, na hivyo anataka kuwa na mazingira mazuri ya kufanya hivyo akiwa na Stars.
Simba na Yanga zimeipinga vikali kanuni ya kusajili wachezaji watano wa kigeni, kwa madai kuwa inawaharibia mipango yao waliyokuwa wamejiwekea kuanzia awali, kwani walitakiwa kupewa muda mrefu wa kujiandaa kufanya hivyo.
Kabla TFF hawajatangaza kanuni hii, timu zote za ligi kuu zilikuwa zikiruhusiwa kusajili wachezaji 10 wa kigeni, na kutakiwa kuwatumia watano katika mchezo mmoja.
Mwisho
No comments:
Post a Comment