
Mafanikio yoyote nyuma yake huwa kuna kionjo cha fedha! Zinaheshimiwa kwa sababu zina nguvu! Wapendanao wengi waliachana baada ya mmoja kuingiwa na tamaa ya kutaka zaidi ya kile anachokipata kutoka kwa mwenzi wake. Binadamu wote wangekuwa na uwezo sawa, uaminifu ungekuwa na kiwango cha juu, na neno “penzi la kweli” lingeleta maana.
Pesa imesababisha siku hizi mapenzi yasiwe na nguvu pale kwenye ukata. Wengine wamekuwa na woga wa kujishughulisha na aina fulani ya watu, kwa kuona kwamba wenye pesa wakiamua, watawanyang’anya. “Mimi mwanamke mzuri simtaki, uwezo wangu mdogo, nitanyang’anywa!” Ni kauli ya unyonge na inaumiza!
Ukweli ni kwamba palipo na mgogoro wa pesa, salio halitoshi na madeni kuongezeka, husababisha athari hasi kwenye uhusiano wako wa kimapenzi! Haijalishi ni kwa kiasi gani wewe ni mwenzako mnapendana. Ni mabadiliko ambayo hayaepukiki na wapenzi wengi yalipowafika, walipena mkono wa kwa heri bila kupenda.
Hii ni kwa sababu unapotoka kwenye maisha ya utulivu, yaliyojaa starehe, kwenda kwenye mabadiliko ya kiuchumi ambayo kila mmoja huwa hapendi itokee, husababisha msongo wa mawazo kwa wahusika na kuchochea uvumilivu ukome haraka. Hivyo basi, penzi huingia mdudu kabla ya kuwa mwanzo wa kutengana.
Inapotokea kwamba kiwango cha uvumilivu kimekuwa finyu kwa wawili wanaopendana, husababisha maudhi ya hapa na pale, kero zisizo na maelezo ya kutosha kutokana na shaka ambayo hutawala fikra za kila mmoja kwenye uhusiano.
Je, unayo imani kwamba tatizo la fedha linaweza kuharibu muungano wako wa kimahaba na mwenzio? Inawezekana lakini siyo kihivyo! Kwa migogoro yote ya pesa uliyonayo leo, haitofautiani na ile ambayo itakufika siku za usoni au mbeleni. Maumivu ni ya wawili, ni vizuri kuvumiliana, kushikamana ili kuvuka vizingiti.
Kitu muhimu cha kufanya ni kushirikiana, kuepuka kugeukana na kucheza mchezo wa lawama. Huyu amuone mwenzake ndiyo chanzo cha tatizo. Zingatio ni kwamba mapenzi yakishamiri, kwa kiasi fulani hupunguza mawazo yanayosababishwa na ukata.
Hali imekuwa mbaya, ni sawa ila zingatia kuwa vyovyote mnavyojikuta mpo kwenye mazingira tata kiuchumi, mnapaswa kushirikiana mpaka pale yatakaponyooka. Hii inajumlisha kupanga bajeti ya vitu na kujibana kuliko mwanzo, pia kujitahidi kutafuta bidhaa za gharama nafuu, yote hiyo ni ili mfurahie maisha licha ya ukata unaowakabili.
Kushirikiana katika kutafuta vitu vyenye sura ya kimahaba, kutoka ‘out’ kwenye maeneo ambayo hayagharimu pesa nyingi, ni muhimu mno katika kuweka hai uhusiano wako, pale unapobeba tafsiri ya “mambo magumu.”
Ni aibu kizuizi cha pesa kusababisha mtengane. Ni muhimu mambo ya fedha yakapata kujadiliwa na ninyi wote pamoja. Ila mtikisiko huo hauruhusiwi kuwafanya muwe wazembe kujenga penzi endelevu. Ikitokea ni dhambi kubwa! Hamna fedha, lakini yapo mambo ambayo mkiyafanya mtafurahi, ingawa hayatogusa mfuko wa yeyote kati yenu.
Mfano, kukaa nyumbani na kuangalia muvi nzuri itawagharimu kiasi gani? Fikiria kwamba wewe na yeye mmeketi vizuri kitini sebuleni, mnazungumza mambo yenye kuleta mwanga wa kimaisha, huku matukio ya filamu yakiteka hisia zenu.
Maisha yametofautiana, inawezekana ‘cha kuonea’ hakipo nyumbani, lakini hiyo siyo ishu! Kila mtu anahitaji kupewa elimu ya mapenzi, iwe mjini au kijijini. Kwa maana hiyo, anaweza kuketi faragha na mwenzi wake na kusimuliana hadithi za kimapenzi.
Yapo mazingira mazuri yenye hewa safi, fukwe mbalimbali, bustani na kadhalika. Yote hayo ni maeneo ambayo unapaswa kuyatumia na mwenzi wako kuhakikisha furaha haipotei. Lingine ambalo linaweza kufanyika bila kuwagharimu kutoboka mifuko ni kupika chakula kizuri cha usiku ambacho kitakupendeza wewe na mwenzi wako.
Furaha kidogo huyeyusha maudhi na msongo wa mawazo! Kula ‘msosi’ mtamu, kuchombezana kwa hadithi za hapa na pale ni kitu maalum sana. Inawezekana pia, kutoka ‘out’ na kwenda kujumuika pamoja kiwanja tulivu, kupata ‘dinner’ pamoja, huku mkiburudishwa na muziki laini.
Kuna mambo mengi ya kufanya, ila pointi ya msingi ni kuwa makini na uhusiano wako na kuhakikisha huyumbishwi na matatizo ya kifedha. Hustahili kuchachawa, kuna wakati wa kupigana kwa ajili ya pesa lakini pia kipo kipindi cha kudumisha penzi.
Hisia zako kwenye pesa na mapenzi ni muhimu lakini si busara kuchanganya moja kwa lingine. Wiki ijayo tutaendelea na dondoo muhimu zitakazokuwezesha kukamilisha furaha yako ya kimapenzi wakati mambo ya kifedha yanapokwenda ndivyo sivyo.
Itaendelea wiki ijayo...
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment