Mara zote mbili aliangushwa na rais anayemaliza muda wake, Amani Abeid Karume, ambaye aliingia Ikulu ya Zanzibar mwaka 2000 na kufanikiwa kutetea kiti chake mwaka 2005.
Dk Shein alizaliwa Machi 13, 1948 katika Kijiji cha Chokocho kilicho wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba.
Alipata elimu ya msingi na sekondari kisiwani Unguja. Alisoma katika Shule ya Wavulana ya Gulioni kati ya mwaka 1956 na 1964 na alijiunga na Shule ya Sekondari ya Lumumba mwaka 1965 na kumaliza mwaka 1968.
Mwaka 1969 alikwenda nchini Urusi kujiunga na Chuo Kikuu cha Vorenezh kwa kozi ya maandalizi ya mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu. Baada ya kumaliza kozi hiyo (mwaka 1970) alijiunga na Chuo Kikuu cha Odessa kusomea masuala ya tiba ya magonjwa ya binadamu (medical biochemistry) hadi mwaka 1975 alipohitimu na kutunukiwa shahada ya uzamili.
Mwaka 1984 alienda Uingereza kuchukua masomo ya shahada ya juu ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Newcastle. Alihitimu masomo hayo mwaka 1988 na kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD). Dk Shein alipata pia mafunzo mengine mbalimbali katika fani ya tiba na uongozi ndani na nje ya nchi.

Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Dk Gharib Bilal akiwassili katika ukumbi wa White House mjini Dodoma tayari kwa kikao cha CCM
Aliwahi kufanya kazi katika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Zanzibar na kwa nyakati tofauti tangu mwaka 1969. Aliwahi kuwa karani katika Wizara ya Elimu, Zanzibar na Msaidizi wa Katibu Mkuu ‘B’ katika wizara hiyo.
Aliwahi pia kuwa mkuu wa Idara ya Huduma za Maabara katika Wizara ya Afya, Zanzibar mwaka 1979 na kudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 1984.
Mwaka 1989 aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Patholojia katika Wizara ya Afya na mwaka 1991 aliteuliwa kushika nafasi ya meneja wa Mradi wa Kudhibiti Ukimwi, Zanzibar huku akiwa na majukumu mengine ya kutoa ushauri kwa wizara. Aliingia kwenye siasa tangu akiwa mwanafunzi.
Alijiunga na Umoja wa Vijana wa chama cha Afro Shiraz tangu akiwa shuleni na mwaka1968 aliteuliwa kuwa katibu wa habari wa Umoja wa Vijana wa Afro-Shiraz kwenye Shule ya Sekondari ya Lumumba.
Dk Shein aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Oktoba 1995 na Novemba aliapishwa kuwa Naibu Waziri wa Afya Zanzibar. Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Jimbo la Mkanyageni, kisiwani Pemba.
Mwaka huohuo aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Katiba na Utawala Bora wa SMZ. Alidumu katika wadhifa huo hadi Julai 2001 alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kiti hicho kuachwa wazi na Dk Omar Ali Juma aliyefariki ghafla.
Naye Dk Bilal ni mwanasayansi wa nyuklia aliyejikita kwenye fizikia. Amewania nafasi ya urais Zanzibar mara tatu bila mafanikio. Alingara kwenye siasa za Zanzibar mwaka 1995 wakati huo rais akiwa Dk Salmin Amour ambaye alimpandisha na hatimaye kuwa Waziri Kiongozi.
Mwaka 2000 aliingia kwenye kinyanganyiro cha kuwania urais kwa tiketi ya CCM na alitoa upinzani mkali kwa Rais Karume. Katika kura zilizopigwa Zanzibar, Dk Bilal aliongoza lakini katika kikao cha halmashauri kuu kilichofanyika mjini Dodoma alidondoshwa na Karume.
Mwaka 2005, Dk Bilal aliamua kugombea tena, lakini Kamati Kuu ya CCM ikamuomba kuondoa jina lake kabla ya kufikishwa kwenye kikao cha halmashauri kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Mwaka huu, Dk Bilal amejitosa kwa mara ya tatu na safari hii akikwaana na kizingiti kingine, Dk Shein.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment