
16th August 2010
Aliyekuwa Mbunge wa Tarime, mkoani Mara kwa tiketi ya Chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema), Charles Mwera (pichani), amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF) kwa kile alichodai kuwa hakutendewa haki katika uteuzi wa mgombea wa chama hicho kupitia kura za maoni.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akitambulishwa kwenye chama hicho jana, Mwera alidai kuwa ameamua kukihama chama hicho kwa lengo la kuleta maendeleo katika jimbo hilo.
Mwera alisema amehama chama hicho baada ya kufanyiwa mizwengwe na rushwa kutawala kwenye kura za maoni za chama hicho zilizofanyika hivi karibuni na kubwagwa.
“Nina msimamo wa kutenda haki kwa wananchi wa Tarime, nimeamua kukihama chama cha Chadema kwa kuwa hawakunitendea haki katika uteuzi wa mgombea ubunge wa jimbo hilo... nahamia CUF ili niendelee kuwafanyia wananchi maendeleo” alisema Mwera.
Mwera alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo Jimbo la Tarime mwaka 2008 kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Chacha Zakayo Wangwe. Akimkabidhi kadi ya kujiunga na CUF, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Juma Duni Haji, alimpongeza Mwera kuhamia chama hicho.
“Nategema utapigania haki ya wananchi kwa kupitia chama cha CUF... karibu sana Mwera,” alisema Duni Haji.
Licha ya kuwa mbunge katika Bunge lililomaliza muda wake Agosti Mosi, mwaka huu, Mwera pia alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilayani Tarime.
No comments:
Post a Comment