
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.
Na Mwandishi WetuChama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelalamikia na kudai ni mateso makubwa kwa wagombea wao kupata fomu za gharama za uchaguzi katika majimbo yao.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema juzi kuwa wagombea wao wa nafasi za ubunge na udiwani sehemu mbalimbali nchini wamekuwa wakimpigia simu na kulalamika kwamba hawajapatiwa fomu hizo.
“Tumepigiwa simu kutoka kwa wagombea wetu na wanalalamika kuwa hawajapata fomu za kuainisha gharama za matumizi yao kwenye uchaguzi lakini wapinzani wetu wagombea wa CCM tuna taarifa kuwa wamepewa nahii kwetu ni hujuma inayofanywa na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi,” alidai Mnyika.
Alisema sasa wameitaka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini izingatie kuwa mchakato huo wa kupata fomu hizo umecheleweshwa na serikali hivyo wameiomba isogeze mbele tarehe ya mwisho ya kurudisha fomu ama iache kabisa kuweka pingamizi kwa wagombea ili kuepusha wagombea kuenguliwa kwa mapingamizi.
Aliongeza kuwa chama chake kiliwasiliana na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi na wamekuwa wakieleza kuwa hawajapokea fomu hizo kutoka kwa msajili au Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC).
Aliishauri ofisi ya msajili kuchukua jukumu la kusambaza fomu hizo badala ya kuviachia vyama vya siasa ama watendaji wengine.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment