
Aidha, niwape pole Waislamu wenzangu ambao wako katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Mungu awape nguvu na awaepushe na vishawishi ili mwisho muweze kupata kile mlichokitarajia kutoka kwake,Inshaallah!
Wiki hii mpenzi msomaji wangu nitajaribu kujibu baadhi ya maswali ambayo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara. Kuna ambayo nitayajibu katika makala nitakazokuwa nikiziandika katika siku zijazo na haya yafuatayo ni machache tu kati ya hayo.
Sitaki kumkosa lakini anataka tufanye mapenzi mwezi mtukufu, nifanyeje?
Uncle Zekaima, kwanza pole kwa jukumu zito ambalo umejipa la kutuelimisha katika mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Naitwa Zamda wa Morogoro, ninaye mpenzi wangu ambaye naye ni Muislam. Kabla ya kuingia kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwanaume huyu amekuwa akipenda sana kufanya mapenzi, yaani haiwezi kupita wiki bila kukutana. Kwa kuwa nilikuwa nampenda sana sikuwa tayari kumkwaza.
Tumeingia mwezi mtukufu, mwenzangu hataki kufunga lakini pia akanipa angalizo kuwa, endapo nitafunga niwe tayari kuharibu funga yangu kwa siku moja moja kwani hataweza kuvumilia kwa muda wa mwezi mzima laasivyo niwe tayari anisaliti? Kusema ukweli kutoka moyoni mwangu, nampenda sana mwanaume huyu kwani achilia mbali kwamba ni mtu asiyeiheshimu dini yake, ana kila kigezo cha kuwa mwanaume wa maisha yangu? Naomba unishauri katika hili!
Uncle Zekaima anajibu: Kwanza kabisa nataka niseme kwamba, kwa jinsi ninavyojua hakuna dhambi kubwa anayoipata Muislamu kama kuzini ndani ya mwezi huu. Lakini pia utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakubali mapenzi yakugombanishe na Mungu wako.
Kwa hili la huyu mpenzi wako inavyoonekana siyo mtu anayejali na kuiheshimu imani yake. Ingekuwa ni Mkristo sawa lakini kama ni Muislam na bado anataka kukuharibia funga yako, huyo hafai! Ni bora umkose tu kuliko kukubali kufanya naye mapenzi katika kipindi hiki.
Nasema hivyo kwakuwa, Mungu ndiye anayepanga katika kila kitu, yawezekana hakupanga huyo awe mwanaume wa maisha yako hivyo muache aende huku ukiamini kuwa yule mwenye mapenzi ya kweli anakuja baada ya huyu. Mheshimu mpenzi wako lakini yule asiyependa kuiheshimu dini yake na Mungu wake mdharau.
Nimechelewa kushika mimba kamzalisha rafiki yangu!
Naitwa Sheila, nilijaaliwa kumpata mwanaume ambaye alikubali kunioa. Baada ya kuingia katika maisha ya ndoa, mume wangu huyu akanieleza kuwa, ana hamu kubwa ya kuitwa baba hivyo tufanye jitihada za dhati za kumtafuta mtoto. Kwakuwa na mimi nilikuwa nikihitaji kuitwa mama, nilikubaliana na mawazo yake.
Siku zikaanza kusogea, mara mwaka ukapita bila mafanikio yoyote. Mume wangu akaanza kuwa na wasiwasi kwamba, yawezekana kati ya mimi au yeye kuna mwenye matatizo ya uzazi. Nilimshauri twende tukapime lakini alionekana kutokuwa tayari kwa hilo. Tukaendelea na maisha yetu kumbe mwenzangu alitafuta njia ya kujijua yuko fiti ama laa kwa kutembea na rafiki yangu.
Ilikuwa vigumu kugundua lakini baada ya muda alikuja kuniomba msamaha kuwa, kampa mimba mtu mwingine ila kiukweli ananipenda mimi. Nilishtushwa na taarifa hizo na kwa hasira nikawa nimerudi kwa wazazi wangu. Wakati niko kwetu, nikaanza kuona mabadiliko nikajihisi ni mjamzito. Nilipokwenda hospitalini kupima nikaambiwa ni kweli nina mimba.
Sikuweza kuamini kile nilichokuwa naambiwa. Hata hivyo, badala ya kuwa na furaha, nilianza kutokwa na machozi nilipokumbuka kuwa, mume wangu kishampa ujauzito mwanamke mwingine. Katika mazingira haya nifanyeje?
Uncle Zekaima anajibu:Inavyoonekana mume wako hana subira na ni mtu anayekata tamaa mapema. Hata hivyo, yaliyotokea yametokea na bado huyo ni mume wako hivyo cha kufanya ni kurudi kwake ili mkaendelee na maisha yenu. Tambua tu kuwa mumeo ana mtoto nje na siyo mke hivyo onesha mapenzi yako yote ili umshike vilivyo.
Naamini maisha yenu yatakuwa mazuri na pia yeye atajirudi hasa pale atakapogundua kuwa amefanya makosa makubwa sana kukusaliti akijua huzai kumbe muda tu ndiyo ulikuwa bado.
Mpenzi wangu anatongozwa sana nahisi siku moja atanisaliti.
Miongoni mwa wanaume waliobahatika kupata wapenzi sahihi mimi ni mmoja wao. Kwanza ni mzuri wa umbo, sura na tabia. Pia ni mcheshi kiasi kwamba, anapendwa na kila mtu. Hucheka na kila mtu lakini tabia yake hiyo imenifanya niwe na wasiwasi kwake.
Wanaume wengi wamekuwa wakimtongoza na kila ambaye amekuwa akimtokea huja kuniambia huku akidai kuwa yeye ana msimamo na kamwe hawezi kunisaliti.
Kinachonichanganya ni idadi ya wanaume wanaomtokea kwa siku tena wengi wakiwa wamejaaliwa pesa na muonekano mzuri.”Unajua mpenzi wangu kwa huu ucheshi wangu wapo wanaume ambao huhisi nawapenda wakati kiukweli nafanya hivyo ili kutengeneza uhusiano nao mzuri wa kikazi,”huniambia hivyo mpenzi wangu.
Hofu yangu ni kwamba, yawezekana siku moja akazidiwa nguvu akashawishika na kunisaliti. Nifanyeje ili kukabiliana na hali hii.
Amiri Sufian wa Dar-es-Salaam
Uncle Zekaima anajibu:Kikubwa ambacho naweza kukusaidia ni kujenga mazingira ya kumuamini mpenzi wako kwani kama unamuamini huna sababu ya kuhisi anaweza kukusaliti. Hata hivyo, unatakiwa kuzungumza naye na kumuomba kuacha kuwachekea wale anaohisi ukaribu wao kwake ni njia ya kumuomba penzi.
Akishawajua anatakiwa kuwakwepa na kutocheka nao kwani hata kama anasema ana msimamo, anaweza kujikuta anakusaliti hivi hivi kwakuwa wapo wanaume ambao wakidhamiria jambo watafanya kila wawezalo kulitimiza.
Kwa maana hiyo basi, mshauri kuwa kama kweli anakupenda na anataka kukujengea mazingira kuwa hawezi kukusaliti, ajiweke mbali na wanaume wanaomtongoza na hata kama anataka kutengeneza uhusiano mzuri nao wa kikazi, awaheshimu tu na wakimtongoza aoneshe amevunjiwa heshima hivyo akasirike na siyo kuwakenulia meno.
No comments:
Post a Comment