
NAAM, kama ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba, ili kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku ambayo yametawaliwa na mapenzi kwa asilimia kubwa.
Nina imani waumini wote wa dini ya kiislamu wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wote walio katika mfungo wa mwezi huu nawatakiwa mfungo mwema.
Leo nataka tuzungumzie kitu kimoja kuhusiana na baadhi ya watu kutaka kuishi dunia ya peke yao, kutokana na upumbavu wao. Kumekuwa na baadhi ya mambo ambayo mtu hufanya na kupata tafsiri mbaya katika jamii.
Kwa mfano kuvaa mavazi ya kujidhalilisha hasa kwa wanawake kutembea nusu uchi au mtoto wa kiume kutoga masikio na kusuka nywele kama mwanamke. Watu hao wakikanywa utawasikia hebu tuacheni au niacheni nilivyo, haya ndiyo maisha yangu.
Huenda mfanyaji ni limbukeni kwa kile alichokifanya bila kujua anachokifanya kinapokelewa vipi katika jamii. Wanadamu tumepewa akili kufanya mambo yanayokubakila katika jamii hasa akiwa mtu maarufu ambaye jamii nzima inamtazama wewe.
Nani alikueleza kuna dunia ya wapumbavu ambayo haina kiongozi anayeweza kukemea mabaya na kusifia mazuri. Kila kiumbe hupitia hatua toka kuzaliwa mpaka utu uzima huku wazazi wakijitahidi kumlea katika malezi bora ya heshima na taadhima.
Lakini kumezuka tabia za ajabu kwa vijana wa sasa ambao nao wameunda dunia yao ya kutembea uchi kwa wanawake kwa wanaume kujigeuza nusu wanawake kukosa heshima mbele za watu. Watoto wadogo wa shule za sekondari kukosa heshima kwa watu wazima.
Wakikemewa utasikia, usiingilie maisha yangu haya ndiyo maisha ninayoishi. Mmh, hii inatisha, lakini chanzo cha yote ni nani?
Ni wazazi ambao wamesahau malezi waliyolelewa na wakubwa zao yalikuwaje, kuna baadhi ya viungo vya mwanamke ni aibu kuonekana. Lakini leo hii kuona nguo ya ndani, shanga au sehemu za siri, limekuwa ni jambo la kawaida.
Lakini nataka kuwaeleza, hakuna dunia ya wapumbavu ambayo siku moja mtaishi, zaidi ya mwisho wa siku iwe kilio na majuto. Tabia na muonekano wa mtu ndiyo sura halisi ya maisha yake.
Usifikiri usipojirekebisha leo ukikomaa utarekebishika, kila jambo baya hujenga kiburi moyoni na mwisho wa siku aibu hupotea na kuishi kama mnyama usiye jua baya lipi na zuri ni lipi. Na kwa tabia hiyo mwisho wa siku utakosa mtetezi.
Bado mna nafasi ya kuishi kama wenzenu wenye heshima huku mkiamini kabisa tabia njema ni keki isiyooza. Ukiona unachokifanya kila mtu anakinyooshea kidole kiache mara moja hakifai siyo kusema haya ni maisha yangu. Huwezi kuishi dunia ya peke yako. Jiheshimu utaheshimiwa, heshima inaanzia kwako.
Kwa haya machache tukutane wiki ijayo.
Simu: +225 713 646500 E-mail:ambedkt@yahoo.com
1 comment:
Mbona Babu anatoa hizi nakali nzuri kwa Kiswahili , Halafu Picha zote ni za watu weupe? Kulikoni Au anamaana watu weupe tu ndio wanaojuwa mapenzi au ?
Post a Comment