Huku taifa likipata mshtuko kufuatia mgombea u-Rais wa Tanzania kwa ‘leseni’ ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kutaka kuanguka jukwaani akihutubia maelfu ya wakazi wa Dar siku ya kuzindua kampeni ya chama hicho, Sheikh Yahya Hussein ameweka kweupe sababu ya tukio hilo.
Tukio hilo lilijiri Jumamosi ya Agosti 21, 2010 majira ya saa tisa na dakika ishirini alasiri, kwenye Viwanja vya Jangwani jijini Dar na kuzua hali ya simanzi na majonzi kwa watu waliohudhuria huku wakiwa hawajui cha kufanya.
Akiongea na Ijumaa Wikienda, muda mfupi baada ya tukio hilo, Sheikh Yahya ambaye ni Mnajimu maarufu Afrika Mashariki, alisema kuwa, kilichomfika mgombea huyo wa CCM ni kuonesha dalili za ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 31, 2010.
Sheikh alisema kuwa, tukio hilo lilitokea kama ishara ya mgombea huyo kuibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya wagombea wengine.
“Hakuna lingine, ile ni dalili ya ushindi mkubwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ndiyo maana,” alisema Mnajimu huyo.
Alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, kitakachotokea, siku ya uchaguzi, kila mpiga kura atakapoingia kwenye chumba cha kuchagua, akili yake itamkumbuka JK, “kwa hiyo lazima mpiga kura atampigia yeye,” alisema Sheikh Yahya.
Hata hivyo, Sheikh Yahya akawatoa wasiwasi Watanzania kwa kusema: “Yule (Kikwete) atapiga kampeni sawasawa mpaka mwisho na afya njema tu.”
...Mmoja wa wanachama wa CCM
Lakini wakati Mnajimu huyo akiweka bayana hilo, Daktari wa magonjwa ya binadamu, Dk. Leopard Mwinuka alisema kuwa, kuna sababu karibu tatu zinazosababisha mtu kuanguka ghafla.Alisema, uchovu kwa mtu anayefanya kazi kwa muda mwingi bila kupumzika, nayo ni sababu moja wapo.
“Kama mtu anafanya kazi kwa muda mrefu halafu mapumziko ni hafifu, uwezekano wa kuanguka akiwa amesimama kwa zaidi ya dakika kumi ni mkubwa,” alisema Dk. Mwinuka.
Aliongeza kuwa, mshtuko nao huchangia mtu kuanguka ghafla.
...Mwenye shati jeupe alidaiwa kunaswa na bastola bandia
Akifafana kuhusu mshtuko, mtaalam huyo alisema kuwa, si lazima mhusika awe ameshtuliwa na kitu au mtu, bali wakati mwingine mwili hushtuka wenyewe.“Mshtuko pia husababisha mtu kuanguka, lakini si lazima mtu ashtuliwe na kitu, kwani wakati mwingine mwili hushtuka wenyewe,” alisema Dokta huyo.
Aliongeza kuwa, kushuka kwa Sukari mwilini pia inaweza kuwa chanzo cha mtu kujikuta anaanguka endapo amesimama kwa muda mrefu.
“Sukari nayo ikishuka, kama mtu amesimama kwa muda mrefu anaweza kuanguka ghafla. Lakini katika hili la mheshimiwa Rais naamini ni uchovu tu. Unajua JK anachapa sana mzigo, we fuatilia tu utakubaliana na mimi,” alisema.
Aliongeza kuwa, katika yote, mtu anayeanguka kwa uchovu mara nyingi baada ya dakika chache ana uwezo wa kuendelea na shughuli zake kuliko yule anayeanguka kwa Sukari kushuka au mshtuko.
Wakati huo huo, kufuatia tukio hilo, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies Of God (Mikocheni B), Getrude Rwakatare ambaye alikuwepo eneo la tukio, alipanda jukwaani na kuanza kukemea roho ya machafuko huku akiirejesha amani ya Mungu eneo hilo mpaka pale Katibu Mkuu wa CCM aliposimama na kuwatuliza watu akisema JK atarejea akiwa na afya njema.
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa CCM, Richard Tambwe Hizza alisema tukio la Kikwete lilisababishwa na uchovu na swaumu.
Mauzauza zaidi yalitawala eneo la tukio baada ya mwanaume mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja, kudakwa jukwaani kwa viongozi na kuhisiwa ni mganga wa kienyeji huku Itifaki ikiwa haimtambui.
Vyombo vya Dola vilimdaka mtu huyo na kuondoka naye kusikojulikana ambako inaaminiwa alihojiwa.
Mbali na mtu huyo, kijana mwingine ambaye pia jina lake halikuweza kunaswa haraka, alikamatwa juu ya jukwaa na kudhaniwa anataka kufanya tukio baya baada ya kukutwa na bastola ambayo baadaye ilibainika ni ya bandia.
Kijana huyo, pia aliondolewa eneo la tukio na ‘difenda’ la polisi.
HABARI KWA HISANI YA GLOBAL PUBLISHERS




No comments:
Post a Comment