
Ukijaribu kuchunguza utabaini kuwa, wengi huchukua muda mfupi sana kabla ya kuachana kwasababu mbalimbali lakini mbaya zaidi wapo wanaoachana wakiwa bado wanapendana. Yaani wanaachana mioyo yao ikiwa inawauma, ndiyo maana nikaona kwa uchache leo nijaribu kugusia mambo haya matatu ambayo ukiyafanyia kazi katika maisha yako ya kimapenzi ya kila siku, faida yake utaiona.
Kwanza kabisa, epuka kuwa mbishi hata katika jambo ambalo hutakiwi kubisha. Watu tunatofautiana, kuna wengine wana tabia ya ubishi hata kama jambo linalozungumziwa halistahili ubishi. Kama utakuwa na tabia hiyo basi ni vyema ikaishia kwa wengine lakini sio kwa mpenzi wako.
Unapokuwa na tabia ya kubishana na mpenzi wako hata katika kile ambacho hakistahili kubisha, unakaribisha mazingira ya kuwepo kwa ugomvi ambao unaweza kulijeruhi penzi lenu.
Kama kweli unataka kuona uhusiano wenu unakwenda vizuri jifunze ukweli kwamba siyo kila wakati unaweza kuwa sahihi, kuna wakati utakuwa hauko sahihi na inapotokea hivyo basi kubaliana na hali halisi.
Inapotokea umefanya kosa halafu unabisha kwamba hukufanya, inaweza kumpa picha flani mpenzi wako. Wazazi wamekuwa wakitufundisha kwamba, kumbishia mtu aliyekuzidi umri ni dalili za kutokuwa na heshima kwake. Hivyo hivyo kwa wapenzi, unapombishia mpenzi wako inaashiria kuwa humheshimu na kwamba, wewe ni jeuri tabia ambazo ni mbaya sana.
Pili, huyo uliye naye kama kweli unampenda kwa dhati kutoka moyoni mwako, hakikisha unajenga mazingira ya kumuamini lakini pia fanya kila uwezalo kumfanya naye akuamini. Yaani asiwe na wasiwasi na wewe hata chembe.
Uaminifu ni kitu cha msingi sana, unaposhidwa kumuamini ‘honey’ wako mara kadhaa utakuwa unahisi anakusaliti kwa kuwa na mtu mwingine hata kama unavyodhani vinaweza vikakosa ukweli.
Hali hiyo inaweza kukufanya ukakosa raha kila mwenza wako anapokuwa mbali na wewe. Si kukosa raha tu anapotoka ama anapokuwa mbali na upeo wa macho yako bali pia unapokuwa naye unaweza kushindwa kuonesha upendo wako kwake.
Suala la uaminifu limekuwa adimu sana kwa baadhi ya wapenzi hasa katika ulimwengu wa sasa. Ni wachache sana ambao ni waaminifu kwa wapenzi wao. Wengine wakipewa uongo tu kwamba mwenza wake ana uhusiano na mtu mwingine anakubali mara moja hata kama habari hizo hazina ukweli wowote matokeo yake unachukua hatua zisizostahili.
Amini kwamba mpenzi wako ni mwaminifu kwako na jijengee mazingira ambayo na yeye ataamini kwamba wewe ni mwaminifu kwake. Muamini ili naye akuamini. Epuka sana kufanya mambo ambayo yanaweza kumsababishia mpenzi wako akadhani una uhusiano wa kimpenzi na mtu mwingine.
Waweza kufanya hivyo kwa kuwa makini na maneno yako pamoja na matendo yako ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kudhihirisha kwamba sio mwaminifu katika uhusiano wenu.
Kitendo cha kuwa na uhusiano wa karibu na watu jinsia tofauti bila kuwepo na sababu za msingi, kupunguza mapenzi, kutokuwa na heshima ni baadhi ya matendo yanayoweza kuonesha kwamba sio mwaminifu hivyo ni vyema ukaepukana navyo.
Wengi wameachana na wengine uhusiano wao umeshikiliwa na uzi kutokana na kutokuwepo na uaminifu kati yao.
Tatu,usiyasikilize ya watu. Hivi unajua kuna watu wasiopenda kuwaona wenzao wakiwa katika uhusiano wenye furaha? Watu hawa ndiyo wanaosababisha wapenzi wengi kuachana. Maneno ya watu ndiyo yamekuwa yakijenga ama kubomoa hivyo sikushauri kwamba usiyasikilize kabisa ya watu, kuna mambo mengine ambayo unaweza kuambiwa na watu yakawa ya faida katika maisha yako.
Wapo watu ambao wanaweza kukushauri juu ya mambo mbalimbali si vizuri ukawapuuza, wasikilize na pima ushauri wao, angalia kwamba unaweza kukusaidia ama laa. Unapofikia hatua ya kuwa na mpenzi ina maana umepevuka kiakili, unaweza kutambua lipi sawa na lipi siyo sawa.
Kabla ya kumalizia mada hii niseme kwamba kumekuwepo na malalamiko ya mara kwa kwa wanandoa na wapenzi ambao wote wanafanya kazi juu ya uaminifu. Tutambue kwamba, ikitokea bahati mkaoana au mkawa wapenzi na wote mnafanya kazi, uvumilivu wa hali ya juu unahitajika, kinyume chake hamuwezi kudumu.
Ni hayo tu kwa leo, tuonane tena wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake