Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Saidi amefanya tukio ambalo halijawahi kutokea baada ya kuandaa sherehe kubwa ya harusi akisema anakwenda kumwoa mwanaume mwenzake kwa madai kwamba, amezidi umbea, Risasi Mchanganyiko lina kila kitu kibindoni.
Baikoko kutoka Tanga.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Septemba 17, 2010 Sinza ya Kumekucha jijini Dar es Salaam jirani kabisa na hoteli ya Lion ambako mwanaume aliyedaiwa kufanyiwa kitendo hicho (jina tunalo) anaishi.Msafara wa magari ya kifahari yapatayo kumi na tano yaliwasili nyumbani kwa mwanaume huyo ndani yake kukiwa na waalikwa walioonekana kuwa na furaha za shamrashamra hizo.
Msafara huo ulipofika nje ya nyumba ya mwaname huyo mwenye mke ulisimama huku matarumbeta yakipulizwa na watu wakiserebuka kwa ngoma ya Baikoko iliyokodishwa toka jijini Tanga.
Hata hivyo, ilidaiwa kwamba mwanaume huyo ambaye bado kijana alipochungulia nje na kuona wageni akiwemo ‘bwanaharusi’ aliingia mitini kwa kutumia mlango wa nyuma kwani toka jana yake alishanyetishiwa kuwepo kwa ‘ndoa’ hiyo ya aina yake.
Mpambe wa 'bwana harusi'.
“Jamaa alichungulia dirishani, alipoona msafara ukifika nyumbani kwao akatimua mbio kwa kupitia mlango wa nyuma, ikabidi tumueke bibi harusi wa bandia ili kumwakilisha.” kilisema chanzo.Akiongea na waandishi wetu eneo la tukio, mmoja wa wageni waalikwa (hakupenda kutaja jina lake) alisema kuwa, wamealikwa katika sherehe ya ‘ndoa’ ya kijana huyo kwa lengo la kumshikisha adabu na kuachana na tabia yake ya ambea mtaani anakoishi.
“Ndiyo, tumekuja kusherehekea harusi ya rafiki yetu Saidi, ni kweli anaoa leo, hii itampunguzia jamaa tabia ya umbea si unaona hata zawadi za Bi harusi tunazo,” alisema mwalikwa huyo ambaye alikuwa ameshikilia sidiria na pete mkononi.
Akifafanua zaidi, alidai kuwa, kijana huyo ana tabia mbaya sana, kwani kila akimkuta mwanaume mume wa mtu amekaa na mwanamke yeye humpigia simu mke na kumnyetishia ishu nzima.
Akasema: “Dawa ya wambea kama hawa ni kuolewa tu, aende akaishi ndani ya nyumba kama mke.”
Hata hivyo, pamoja na ‘mwolewaji’ huyo kuingia mitini sherehe ziliendelea nje ya nyumba kwa ngoma huku ratiba za chakula zikifanyika kama kawaida.
‘Bwanaharusi’ aliyetarajiwa ‘kumuoa’ kijana huyo alipoulizwa kama kweli alikuwa na nia hiyo alikiri na kuongeza kuwa, ndiyo maana aliamua kufanya sherehe kubwa kama ile.
“Ndiyo nimekuja kuoa leo, nataka nikiondoka hapa niwe na mke wangu, nimekamilisha mipango yote ya harusi,” alisema.
Alisema kuwa, amekuwa akigombana na mkewe kila mara akimshutumu kwamba, alikuwa mahali na mwanamke lakini alipofuatilia kwa undani, wasamaria wema kwake wakamtonya kuwa, kijana huyo ambaye awali walikuwa marafiki na hukaa naye beneti ndiye anayemwambia mkewe kuwa mumewe yupo na ‘nyumba ndogo’ mahali.
Aliongeza kuwa, alipania kufanya hivyo na alishakusanya michango ya watu wakiwemo marafiki ili kufanikisha sherehe hiyo ambayo alidai kuwa, kama angemkuta ‘mkewe’ huyo ingekuwa ya kifahari.
Naye Shehe ambaye alitegemewa ‘kuunganisha’ wawili hao, Abdallah Mohamed alisema kuwa, alifika eneo hilo kwa nia ya kufungisha ndoa hiyo ya wanaume kwa sababu ya mabadiliko ya maendeleo ya kisasa duniani.
Habari zaidi katika eneo la tukio zinapasha kuwa, Pedeshee maarufu jijini Dar, Kizaizai yeye alichangia shilingi Laki tano ili kufanikisha sherehe hiyo ambayo Bajeti yake iligonga Shilingi milioni moja za Kibongo.
Pete ya uchumba na ndoa.
Ili kusikia toka upande wa pili, Risasi Mchanganyiko, Jumatatu mchana lilimpandia hewani mwanaume huyo ambaye mkewe inasemekana aliangua kilio kwa tukio hilo, lakini simu yake ya mkononi iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.Baadaye alipopigiwa tena, hakuwa hewani tena hali iliyotafsiriwa kuwa, huenda simu yake iliishiwa chaji au aliizima kwa sababu zake mwenyewe.
Kutoka mezani kwa Mhariri: Tunaamini kuwa, njia zilizotumika kukomesha tabia inayodaiwa kuwa inafanywa na kijana huyo si sahihi, kwani mitaani kuna Wajumbe wa Nyumba Kumi na Serikali za Mitaa, Saidi alitakiwa kwenda huko kutoa malalamiko yake kama kweli ana ushahidi wa ndoa yake kuvurugwa na kijana huyo.
Chanzo GPL




No comments:
Post a Comment